Habari Mseto

Afueni kwa Jaji Mwilu kesi ya kumtimua ikisitishwa

November 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU Jaji Mkuu Philomena Mwilu alipata afueni Ijumaa Mahakama Kuu ilipozima hatua ya Tume ya Kuajiri Watumishi wa Idara ya Mahakama (JSC) kuanza kusikiza kesi inayoomba atimuliwe kazini kwa kukaidi maadili ya kazi.

Jaji James Makau alitupilia mbali ombi la JSC la kutaka kesi mbili alizoshtakiwa Jaji Mwilu na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) zianze kusikizwa.

Jaji Makau aliyezima hatua ya JSC kupitia kwa wakili Paul Muite alisema “maagizo yaliyotolewa Agosti 14 2020 kusitisha kusikizwa kwa kesi za DPP na DCI na JSC zasema zitasilia hadi Mahakama kuu itakaposikiza na kuamua kesi aliyoshtaki Jaji Mwilu.”

Jaji Mwilu anapinga kesi mbili zilizowasilishwa dhidi yake na DPP na DCI za kutaka atimuliwe kazini kwa kupokea mkopo wa Sh315milioni na Benki ya Imperial Limited iliyofungwa.

Jaji Mwilu alilipa mkopo aliopewa na benki hiyo iliyofungwa baada ya kukumbwa na matatizo.

Jaji Mwilu anasema kuwa DPP na DCI wamepotoka kabisa kwa kumfungulia mashtaka kwa kukopa pesa za benki na kuulipa.

“DPP na DCI wanatumia mamlaka yao vibaya kwa kuzindua kesi mbili dhidi ya Jaji Mwilu anayeshikilia wadhifa mkuu katika idara ya Mahakama,” mawakili saba wenye tajriba ya juu wakiongozwa na James Orengo wameeleza mahakama kuu.

Mwaka uliopita majaji watano wa mahakama kuu walitupilia mbali kesi ya uhalifu aliyoshtakiwa Jaji Mwilu mbele ya hakimu mkuu Lawrence Mugambi wakisema “ haina mashiko kisheria kwa vile ilitokana na masuala ya kibiashara ya kibinafsi kati ya naibu wa jaji mkuu na benki.”

Baada ya kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo DPP na DCI waliwasilisha ombi katika JSC wakidai Jaji Mwilu alikaidi maadili ya kazi kwa kutumia makaratasi yaliyo na chapa cha idara ya mahakama kuomba mkopo kutoka kwa benki ya Imperial.

Bw Muite alikuwa ameomba Jaji Makau aamuru kesi hizo mbili zianze kusikizwa na JSC kwa vile muda unayoyoma.

“JSC inataka kusikiza na kuamua kesi hizi mbili kwa haraka ianze kushughulikia mambo mengine ya kusaka mrithi wa Jaji Mkuu David Maraga anayestaafu mwaka ujao,” alisema Bw Muite.

Bw Orengo anayemwakilisha Jaji Mwilu pamoja na rais wa chama cha mawakili nchini Nelson Havi, Bi Aulo Soweto, Okong’o Omugeni, Jack Awele, Daniel Maanzo, Otiende Amolo na Millie Odhiambo miongoni mwa wengine walipinga ombi la Bw Muite wakisema Jaji Mwilu anapasa kuheshimiwa.

Lakini DPP kupitia viongozi wa mashtaka Alexander Muteti na Taib Ali Taib walieleza mahakama kesi hizo zapasa kuamuliwa kwa upesi kwa vile Jaji Mwilu alikaidi maadili.