Afueni kwa Sonko akaunti zake tano kufunguliwa
Na RICHARD MUNGUTI
KAMBA za kisheria zilizomkaza Gavana Mike Sonko zimeanza kulegezwa baada ya agizo akaunti zake tano za pesa zilizokuwa zimetiwa kufuli zifunguliwe.
Jumanne , mahakama ilikiamuru kitengo cha mamlaka ya kutwaa mali zinazoshukiwa zimeibwa (ARA) ifungue akaunti za Sonko.
Mawakili wa Sonko , Cecil Miller , George Kithi na Harrison Kinyanjui waliomba akaunti za Gavana huyu zifunguliwe wakidai “ anateseka na hawezi kukimu mahitaji ya familia yake nay eye binafsi.”
Bw Kinyanjui aliyewasilisha ombi hilo mbele ya hakimu mkuu Martha Mutuku alieleza mahakama ARA imeendelea kufunga akaunti za Sonko kinyume cha sheria.
“ARA haikurudi mahakamani kuomba muda zaidi wa kuchunguza akaunti za Sonko kubaini ikiwa zilikuwa na pesa zinazodaiwa zimetoka kwa umma,” Bi Mutuku alielezwa na Kinyanjui.
Wakili huyo alimdokezea hakimu ARA inatumia vibaya maagizo ya mahakama kwa kuendelea kutia kufuli akaunti za Gavana Sonko.
Bi Mutuku alikubali ombi la mawakili wa Gavana huyo aliyeachiliwa Desemba 11 2019 kwa dhamana ya Sh15milioni alipokanusha mashtaka 18 ya ufisadi.
Hakimu aliamuru,”ARA imekuwa ikitumia vibaya maagizo ya hii mahakama kuendelea kuchunguza akaunti za Sonko,” alisema Bi Mutuku.
Aliamuru mara moja zifunguliwe ndipo mshtakiwa apate fedha za kukimu mahitaji ya familia yake.