• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Afueni kwa Waislamu tarehe ya kusafiri Mecca kusongeshwa

Afueni kwa Waislamu tarehe ya kusafiri Mecca kusongeshwa

Na CECIL ODONGO

Waislamu wametakiwa kutokuwa na hofu wala taharuki baada ya makataa ya kutimiza matakwa yote kusafiri kuenda kuhiji Mecca nchini Saudi Arabia kuongezwa hadi tarehe 31 mwezi huu.

Mwenyekiti wa Muungano wa Hajj na Umra Kenya Sharrif Hussein amesema kwamba muda huo umesongeshwa baada ya barua waliyoiandikia Waziri wa Hajj nchini Saudia Dkt Mohammed Swaleh kukubaliwa na akatoa wito kwa idara ya uhamiaji kujizatiti kuhakikisha kwamba vyeti vya usafiri, pasipoti za mahujaji wote vinakuwa tayari kabla ya makataa hayo mapya.

“Sisi kama Muungano wa Hajj na Umra Kenya tuliona makataa ya awali yangewafungia watu wengi nje ndipo tukamwandikia barua ya kuomba muda zaidi waziri wa Hajj. Tunawaomba wote watakaokwenda hijja waendelee kujitayarisha ili makataa haya mapya yasiwafungie nje,” akasema Bw Hussein.

Aidha, alipongeza usimamizi mpya wa idara ya uhamiaji chini ya mkurugenzi mpya Alex Muteshi ambaye alichukua mahala pa Gordon Kihalangwa aliyepandishwa cheo hadi akawa katibu katika wizara ya usalama wa ndani.

“Tunamwomba Bw Muteshi ajizatiti kuwasaidia Waislamu wote wanaopania kuenda hijja kwa kuhakikisha maombo yao ya pasipoti na mahitaji mengine yanakamilika kwa wakati ufao. Tunafurahi kwamba tayari ameonyesha dalili ya kutusaidia,” akaongeza Bw Hussein

Akizungumzia masuala ya uongozi ndani ya SUPKEM, BW Hussein alipuzilia mbali madai kwamba ofisi ya awali haikutimiza matakwa lengwa kwa jamii ya Kiislamu lakini badala yake akaitaka ofisi ya sasa inayoongozwa na Mwenyekiti Yusuf Nzibo kujizatiti kuunganisha Waislamu wote na kushirikiana nao kikazi kama njia ya kudhihirisha umoja wa dini.

Majuma mawili yaliyopita uongozi wa Supkem ulitangaza Julai 15 kama siku ya mwisho kwa mahujaji wote kutimiza kila hitaji ikiwemo usafiri na gharama nyingine huku.

Kuenda Hijjah ni nguzo ya tano katika dini ya Kiislamu na kila mwenye uwezo anaamrishwa kuitizmiza angalau mara moja maishani.

You can share this post!

Niligonga ng’ombe wala si kuua mwanamke ajalini...

Wanafunzi 500 hutumia choo kimoja, wengi hukimbilia...

adminleo