• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
Afueni ubomoaji wa soko Githurai kusitishwa

Afueni ubomoaji wa soko Githurai kusitishwa

Na SAMMY WAWERU

Wafanyabiashara na wachuuzi wa soko maarufu la Jubilee mtaani Githurai 45, Kiambu, wamepata afueni baada ya serikali kusimamisha ubomoaji wake.

Kulingana na ilani ya barua inayosemekana kutoka kwa halmashauri ya barabara kuu nchini (KeNHA) na iliyokuwa ikisambaa, soko hilo lilipaswa kubomolewa leo, Jumanne Mei 28.

Barua hiyo ilidai vibanda na majengo ya soko hilo vimeundwa katika ardhi ya KeNHA.

Kufuatia kilio cha wafanyabiashara hao Jumatatu kupitia vyombo vya habari, serikali imetangaza kusimamishwa mara moja kwa ubomozi huo ikihoji haijapokea taarifa yoyote. Aidha, walimrai Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati suala hilo wakieleza kwamba Jubilee Market imekuwa kitega uchumi chao.

Msemaji wa Ikulu Kanze Dena alisema serikali haikuwa imetoa amri kama hiyo (kubomolewa kwa soko), kauli iliyowiana na ya serikali ya kaunti ya Kiambu. Bw Ferdinand Waititu ndiye gavana wa Kiambu.

Baadhi ya wafanyabiashara tuliozungumza nao walisema KeNHA pia ilikana kuhusishwa na barua iliyokuwa ikisambaa.

“Tunaishukuru sana serikali kwa kusikia kilio chetu. Soko hili ndilo limetuajiri, unga wa familia zetu hutoka hapa,” akasema mfanyabiashara aliyejitambua kama Mama Muthoni.

Kulingana na Bw Njenga, mmoja wa viongozi, soko hilo lililoko pembezoni mwa Thika Super Highway lina karibu wamiliki 1,800 wa vibanda na majengo.

“Wameajiri wafanyakazi, tungeondolewa tuende wapi? Tena ingekuwa pigo kubwa kwa tunakonunua bidhaa kama vile Gikomba. Hao ni baadhi ya wachache tu wanaotegemea Jubilee Market. Tunakubali soko hili lipo katika ardhi ya KeNHA lakini kuwe na mpangilio maalum wa kutuangazia,” Njenga akaeleza.

“Nimeajiri kijana mmoja, nina watoto wawili na mke, wote wananitegemea. Kutuondoa bila kuoneshwa mahali nitakapoelekea ni kuniongezea taabu,” akasema James Njoroge, muuzaji wa viatu.

Bidhaa zinazouzwa humo kwa wingi ni nguo na vyakula. Majira ya jioni, baadhi ya vibanda hugeuzwa mikahawa, hivyo basi soko hilo linahudumu saa 24 kwa siku.

Wengi wamelisifia kupunguza mtandao wa uhalifu mtaani Githurai, kwa kubuni ajira. Gabriel Ntombura kwenye mahojiano awali alisema aliacha kushiriki visa vya wizi ili kuchuuza maji. “Ninategemea uuzaji wa maji kwa wafanyabiashara na mikahawa,” alisema.

Septemba 2018, soko hilo lilibomolewa chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa polisi. Wakati akituliza ghadhabu za wafanyabiashara, gavana Ferdinand Waititu alisema serikali inapania kuwajengea soko la ghorofa nne na lenye egesho la magari la kisasa.

Mwaka 2017, wakati Rais Uhuru Kenyatta akifanya kampeni za kuhifadhi kiti chake, aliwaahidi kuwa soko hilo litajengwa kwa muundo wa kisasa. Liliratibiwa kugharimu kima cha zaidi ya Sh2 bilioni, na kufikia sasa mpango huo haujaonekana kuzaa matunda.

 

You can share this post!

MURANG’A: Wanawake waliolaani wanao hutakaswa kupitia...

HUDUMA NAMBA: Chifu aamriwa awalipe makurutu wa ziada...

adminleo