Ahmednassir taabani kudai Jaji Ibrahim alihongwa
Na RICHARD MUNGUTI
JAJI wa Mahakama ya Juu Mohammed Ibrahim amempa mwanasheria Ahmednassir Abdullahi siku saba aondoe matamshi kwamba ya ulaji hongo katika kesi ya kuamua mshindi katika uchaguzi wa Ugavana kaunti ya Wajir.
Jaji Ibrahim amesema kuwa Bw Abdullahi alimshushia heshima yake kwa kudai alihusika na upokeaji hongo kabla ya kuamuliwa kwa rufaa ya kupinga uchaguzi wa Gavana Mohammed Abdi Mohamud.
Jaji Ibrahim, kupitia kwa wakili Wambua Kilonzo amempa Bw Abdullahi siku saba amuombe msamaha , aondoe maneno hayo katika mitandao ya Twitter na Whatsup.
“Endapo hautaomba msamaha na kuondoa maneno hayo ya kunishushia hadhi basi sitakuwa na budi ila kuwasilisha kesi katika mahakama kuu dhidi yako (ahmednassir abdullahi),” Jaji Ibrahim alimweleza wakili Abdullahi waziwazi.
Jaji huyo amesema siku moja kabla ya kutolewa kwa uamuzi wa kesi hiyo ya Gavana Abdi , Bw Ahmednassir Abdullahi alimwandikia mlalamishi (jaji Ibrahim) ujumbe katika mtandao wa whatsup akimweleza , “ uvumi na umbea unadai majaji wa Mahakama ya Juu wamepokea pesa kwa magunia na mifuko wamtangaze Abdi mshindi wa uchaguzi wa Ugavana Wajir uliofanywa Agosti 8, 2017.”
Ujumbe huo uliendelea kumsihi Jaji Ibrahim ajiepushe na ulaji mlungula kwa vile ni yeye tu katika mahakama hiyo ya juu ambaye hajatajwa katika kashfa ya hongo.
Ujumbe huo pia ulimhimiza asimame kidete na kukataa kujiunga na majaji waliokuwa wamepanga kumtangaza Abdi mshindi halisi wa kiti cha Ugavana Wajir.
Zaid ya hayo ujumbe ulimsihi Jaji Ibrahim awe na “kumbukumbu kule alikotoka na asiwafuate majaji wengine bila makini.”
Saa chache baada ya uamuzi kutolewa Februari 15 2019 , Jaji Ibrahim anasema Bw Ahmednassir alipeperusha jumbe katika mtandao wa Twitter akidai majaji wa mahakama ya juu walipokea hongo kuhalalisha ushindi wa Abdi kama Gavana wa Wajir.
Ahmednassir alitisha kumwandikia barua Jaji Mkuu David Maraga akifichua jinsi “kila mmoja wa majaji hao wanne alivyopokea hongo.”
“Madai haya yaliharibia sifa majaji wa mahakama ya juu na kuwafedhehesha,” inasema baria hiyo aliyoandikiwa Ahmednassir.
Ahmednassir amesema atawasilisha malalamishi katika tume ya kuajiri wafanyakazi wa idara ya mahakama JSC.
Jaji Maraga alipelekea JSC barua hiyo ya Ahmednassir kushughulikiwa.
Jaji Maraga na Jaji Isaac Lenaola walitofautiana na wenzao Jaji Ibrahim, Jaji Jackton Ojwang, Jaji Smokin Wanjala na Jaji Njoki Ndung’u kwamba Abdi hakushinda kwa njia halali Ugavana Wajir.
Majaji hao wanne walisema mlalamishi Ahmed Abdullahi katika kesi hiyo wangelimshtaki Abdi kwamba hajahitimu kwa shahada ya digirii katika jopo la tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.
Bw Abdullahi ambaye ni gavana wa zamani wa Wajir amewasilisha ombi uamuzi wa majaji hao wanne utathiminiwe upya.
Bw Abdullahi anaomba mahakama ibatilishe uamuzi wa majaji hao wanne wa mahakama ya juu na kuamuru uchaguzi mwingine wa ugavana ufanywe kaunti ya wajir.
Jaji Maraga na Jaji Lenaola walisema Abdi hakuhitimu kuwania kiti hicho cha Ugavana kwa vile hana digirii kama inavtyotakiwa na Katiba na Sheria.