Habari Mseto

Aibu ya machifu kujinufaisha na chakula cha msaada

June 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

By IAN BYRON

Wakazi wa eneo la Uriri, Kaunti ya Mirogi wanalalamika kwamba wasimamizi wa mtaa huo wanajinufaisha na chakula kilichotengewa watu waliokumbwa na njaa kutokana na janga la corona.

Wakazi walimlaumu machifu wa eneo hilo kwa kuchukua mchele uliosambazwa na ofisi za CDF za eneo hilo wiki iliyopita.

Wakazi waliambia Taifa Leo kwamba machifu hao walikuwa wameorodhesha familia zao na watu wa karibu kama watu wasiojiweza huku akiwaacha watu maskini.

Bi Hellen Awino, mwenye umri wa miaka 62 alisema kwamba hakupata chakula hicho licha ya ahadi za chifu huyo kwamba angekuwa mmoja wa waliotengewa chakula hicho.

“Nilitarajia kupata chakula hicho baada ya jina langu kuorodheshwa kama maskini lakini nilikuja kugundua kwamba jina langu halikuwa kwenye orodha,” alisema Bi Awino.

Bw Bernard Ochieng, mkazi mwingine wa Uriri alimlaumu chifu huyo kwa kutosambaza chakula hicho kama ilivyoratibiwa.

Wakazi wa Uriri waliomba mbunge wa eneo hilo Bw Mark Nyamita na mshirikishi wa kaunti hiyo Joseph Rotich wachunguze kisa hicho.

“Bw Nyamita alisema kwamba walikuwa wamepokea madai hayo na wanayachunguza. Tunachunguza kisa hicho na hatua itachukuliwa.”