Habari Mseto

Ajabu ya Chebukati kumtetea Chiloba baada ya kumtimua

November 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati amemtetea aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wa tume hiyo Ezra Chiloba kutokana na sakata ya tenda ya Sh6bilioni, kwenye ununuzi wa vifaa vya kielektroniki vya kukagua wapiga kura na kupeperusha matokeo ya uchaguzi.

Alipofika mbele ya kamati ya bunge kuhusu pesa za umma, Bw Chebukati alisema kuwa uamuzi wa kufanya manunuzi ya moja kwa moja ya vifaa hivyo ulifanywa na makamishna wa tume walipofanya mkutano.

Vifaa hivyo ndivyo vilitumika kuwakagua wapiga kura na kuendesha chaguzi zote mbili za mwaka uliopita Agosti 8 na Oktoba 26.

“Kulikuwa na uchaguzi uliokuwa ukielekea kwa hivyo ilitubidi kufanya uamuzi. Katika hali hiyo, hakukuwa na fursa ya machaguo mengine,” Bw Chebukati akaeleza kamati hiyo iliyoongozwa na mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi.

Alieleza kamati hiyo kuwa mkutano huo wa makamishna ulifanywa mnamo Machi.

“Jukumu la tume ni kutengeneza sera, mpangilio na kukagua namna kazi inafanywa. Tulieleza idara ya usimamizi wa tume kuendelea kutekeleza maanunuzi kulingana na sheria,” akasema Chebukati.

Maelezo ya Bw Chebukati hata hivyo yalikinzana nay ale ya Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa sasa Marjan Hussein ambaye Jumanne alieleza kamati hiyo kuwa Bw Chiloba alifanya manunuzi hayo kivyake bila kumhusisha mtu mwingine.

Tume hiyo ilitumia Sh4,196,300,000 kununua vifaa 45,000 vya KIEMS ambavyo vilitumika katika uchaguzi wa Agosti 8 na Sh2.5bilioni kwa vifaa vilivyotumika kwenye uchaguzi wa marudio Oktoba 26.