Habari MsetoSiasa

Ajenda Nne Kuu: Kamati ya Matiang'i sasa yawalilia wabunge

March 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na IBRAHIM ORUKO

Kamati Tekelezi ya Maendeleo ya Taifa, Jumatatu ilikutana na wenyekiti wa kamati za seneti katika kile kinachoonekana kama juhudi za serikali za kushawishi bunge kuharakisha sheria zinazolenga kufanikisha Ajenda Nne Kuu.

Kamati inayoongozwa na Dkt Fred Matiang’i, ilikutana faraghani na kamati ya pamoja ya seneti katika kile kilichotajwa kama “juhudi za kutafuta ushirikiano katika kupata suluhu la masuala ya kisheria yanayozuia utekelezaji wa miradi ya serikali.”

Kwenye taarifa baada ya mkutano huo, Dkt Matiang’i alieleza hofu yake kwamba, baadhi ya miswada muhimu inayohusishwa na usimamizi wa miradi inakwama Bungeni na kusema kuchelewa kupitisha Miswada hiyo kunafanya wanakandarasi kuteseka na kutoza serikali faini kubwa.

Dkt Matiang’i ambaye ni Waziri wa Usalama wa Ndani, aliwaomba wabunge kuharakisha kupitisha sheria zilizopendekezwa ili kuwezesha utekelezaji wa miradi muhimu inayofadhiliwa na serikali ya kitaifa kote nchini.

Miongoni mwa miswada hiyo ni Mswada wa Utosheleshaji wa Chakula wa 2017, Mswada wa Ujenzi wa miji wa 2017, Mswada wa Unyunyuziaji wa 2017 na Mswada wa Barabara Kenya wa 2017.

“Kamati itazungumza na wadau wote, ikiwa ni pamoja na Baraza la Magavana, kujadili changamoto ambazo zinalemaza utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutafuta mbinu za kuzitatua,” Dkt Matiang’i aliambi kamati.

Kamati yake imetambua matumizi mabaya ya pesa, ukosefu wa kuhusisha umma kikamilifu na usimamizi duni wa miradi kama baadhi ya visiki vya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Spika Kenneth Lusaka, aliambia kamati kwamba, baadhi ya miswada aliyotaja imepitishwa na kuwasilishwa kwa Bunge la Taifa na akaahidi kuhakikisha inayokwama itapitishwa haraka iwezekanavyo.

Mswada wa Utosheleshaji wa Chakula unatoa mwongozo kuhakikisha Wakenya wote wana chakula bora cha kutosha kila wakati.

Ukipitishwa, mswada wa mipango utachukua nafasi ya sheria ya mipango ya 1996 kuhusu mipango, matumizi, na kustawisha ardhi Kenya.