Habari MsetoMakala

AKILIMALI: Kijiji kinachotegemea uchumaji wa chumvi Kilifi

April 2nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na KAZUNGU SAMUEL na EUNICE MURATHE

HUKU jua kali likiendelea kuwachoma bila huruma, wakazi wanaoishi katika ukanda wa kutoa chumvi wa Magarini, kaunti ya Kilifi hawakuonekana kuchoka. Wakiwa na lengo kamili la kujinufaisha kimaisha kupitia kwa kutengeneza chumvi, hakuna kilichoonekana kuwakera wala kuwarudisha nyuma.

Vizavi vilivyopita vyote katika eneo hili vilijishughulisha na kazi ya kuchimba na kutayarisha chumvi, miaka mingi iliyopita.

Tulipofika katika kijiji cha Kadzhuhoni tulikumbana na visima zaidi ya kumi ambavyo wakazi wametayarisha kuvuna  chumvi ili kuendeleza maisha yao. Eneo hilo la Kadzuhoni linapatikana umbali wa kilomita 147 kutoka jijini Mombasa, kwenye barabara kuu ya kutoka Malindi kuelekea Lamu na Garisa.

Baadhi ya visima ambavyo wakazi wametayarisha kuvuna  chumvi katika kijiji cha Kadzuhoni, Kilifi. Picha/ Kazungu Samuel 

Uchumaji chumvi kwa njia ya kienyeji umeendelezwa na wakazi hapa kwa muda mrefu na umerithiwa na vizazi kwa vizazi.

Mmoja wa wakazi wanaomiliki visima hivi vya chumvi Bw Suleiman Wario, alisema kijiji chote cha Kadzuhoni kinategemea shughuli za kuvuna chumvi na kwa kiwango kichache shughuli za kuvua samaki.

 “Tulianza shughuli hii ya kuvuna chumvi katika eneo hili mwaka wa 1968. Mimi ninamiliki visima kadhaa vya chumvi na kuna wakazi ambao huja na kujishughulisha hapa. Kwa siku mara nyengine hupata zaidi ya watu 100 wanakuja hapa kufanya vibarua na kujipatia fedha kuzilisha jamii zao,” akasema Bw Wario.

Wachumaji wa chumvi waonyesha magunia ya bidhaa hiyo. Wanauza gunia moja kwa Sh100. Tani moja ya chumvi inatoshana na magunia 20 ya chumvi. Picha/ Kazungu Samuel

Visima hivi vya Kadzuhoni tuligundua kwamba vinamilikiwa na wakulima watano ambao kwa sasa wameanzisha muungano ili kujaribu kuboresha biashara yao.

 “Mara nyengine biashara inakuwa nzuri kwetu lakini nyakati za ugumu wa biashara, sisi huamua kuja pamoja na kuungana. Kwa sasa tuko na muungano wetu kutetea maslahi yetu,” akasema Bw Wario.

Hata hivyo wakulima hao walitueleza baadhi ya changamoto zao kibiashara ikiwemo kujaa kwa maji ya bahari katika mashimo yao na kutatiza kuzaliwa kwa chumvi.

Wakati wa mawimbi makali na maji mengi baharini, maji hufuata mkondo na kujaa katika mashimo .

Kulingana na Bw Wario, maji ya bahari hupigwa kupitia kwa paipu zilizoundwa maalum katika visima mbalimbali , jambo ambalo alisema linasaidia katika kutayarisha chumvi yao.

Baada ya wiki tatu, chumvi huwa tayari kuvunwa na kutiwa kwa magunia. Picha/ Kazungu Samuel

Tuligundua kwamba utayarishaji wa chumvi huwa na viwango vyake hapa. Kwa mfano kisima cha kwanza huwa kina maji yaliyotoka baharani ambayo hayana chumvi nyingi.

Kisha baada ya siku mbili maji hayo husukumwa katika kisima cha pili huku mvuke wa jua ukitumika kuongeza makali ya chumvi. Shughuli hiyo hufanyika na baada ya wiki tatu, chumvi huwa iko tayari kuvunwa na kuwekwa katika gunia.

Bw Wario aliambia Taifa Leo kwamba yeye hupata kati ya tani  220 hadi 300 kila anapovuna chumvi yake. Yeye binafsi anamiliki visima tisa katika kijiji cha Kadzuhoni.

 “Tuko na maajenti ambao hutoka Nairobi kuja na kununua chumvi yetu hapa. Wao hufika hapa na biashara hii tunaifanya  chini ya muungano wa sisi wamiliki watano,” akasema Bw Wario kabla ya kuongeza

Chumvi hii haijafikia kiwango bora cha kitaifa wala kimataifa. Ndio maana chumvi hii huuziwa maajenti ambao huuza katika kampuni za kuunda chumvi ya kiwango cha juu. Picha/ Kazungu Samuel

“Wananunua gunia moja kwa Sh100 kinyume na awali ambapo tulikuwa tukinunua gunia moja kwa Sh150,” akasema Bw Wario. Tani moja ya chumvi huwa inatoshana na magunia 20 ya chumvi.

Bw Wario alisema kuwa kwa sasa hivi bado hawajapata soko bora la bidhaa yao kwa vile chumvi wanayotoa si ya kiwango cha juu.

Aliongeza kuwa wanapata ushindani mkali kutoka kwa kampuni za chumvi ambazo zimeimarika na ziko na mitambo ya kisasa ya kuchuja chumvi.

“Chumvi yetu haijafikia kiwango bora cha kitaifa na kimataifa. Kwa sababu hiyo bado tunauza chumvi yetu kwa maajenti ambao huuza katika makampuni mengine Nairobi na maeneo mengine. Endapo tutapata usaidizi wa vifaa vya kisasa, tutafika mbali na hata kuanzisha kiwanda chetu chenye vifaa vya kisasa,’ akasema Bw Wario.