Habari Mseto

Alai ndani siku 14 kwa 'kufurahia Al Shabaab wakiua Wakenya'

June 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

Mwanablogu Robert Alai Onyango na afisa wa magereza Patrick Safari Robert Jumatano waliamriwa wazuiliwe kwa siku 14 kwa kuchapisha picha za maafisa wanane wa polisi wa Kenya waliokufa katika shambulizi la kigaidi Juni 15 kaunti ya Wajir.

Hakimu mkazi mahakama ya Milimani Nairobi Bi Sinkiyian Tobiko aliamuru Alai na Safari wazuiliwe kuwasaidia maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi kubaini “uhusiano wao na magaidi wa Al Shabaab waliohusika na shambulizi hilo.”

“Maafisa wa polisi wanahitaji kupewa muda wa kukamilisha uchunguzi kabla ya kuwafungulia mashtaka washukiwa hawa,” alisema Bi Tobiko.

Hakimu alikubaliana na kiongozi wa mashtaka Angela Odhiambo kuwa washukiwa wanapasa kujulikana sababu ya kuchapisha picha za maafisa wanane wa usalama waliouawa katika mtandao wa kijamii wa Alai.

Kiongozi wa mashtaka Angela Odhiambo. Picha/ Richard Munguti

Akiomba wasukumwe ndani , Bi Odhiambo alisema Alai alidhulumu kimawazo familia za maafisa hao walioaga katika shambulizi la kigaidi kwa kuchapisha picha zao katika mtandao wa kijamii.

“Hatua hii ya Alai inabaini kuwa alifurahia kitendo hicho na alikisifia kwa kuchapisha picha za waathiriwa mtandaoni,” alisema Odhiambo.

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema simu za washukiwa hawa zimekuwa zikiwasiliana na watu wanaoshukiwa kuwa magaidi hao wa Al Shabaab.

Bi Odhiambo alieleza mahakama ugaidi umekuwa donda ndugu na kila juhudi yapasa kufanywa kuuangamiza.

Wakili Samson Nyamberi (kulia) akiwa na washukiwa na wakili Angela Mwadumbo (kushoto). Picha/ Richard Munguti

Mahakama ilifahamishwa wanaounga mkono magaidi wa Alshabaab ama visa vya ugaidi wanapasa kuchukuliwa hatua kali.

Mawakili Samson Nyaberia na Angela Mwadumbo walipinga hatua ya kuzuiliwa kwa wateja wao siku 30 wakisema “walinyimwa chakula na simu wanazodaiwa waliwasiliana nazo zimetwaliwa tayari.”

Waliomba kortini iwaachilie kwa dhamana. Ombi lao lilikataliwa na washukiwa hao wakaagizwa walale ndani hadi Julai 3, 2019.