ALI HASSAN KAULENI: Sisi Waislamu tunazo sherehe zetu tunazopaswa kuadhimisha kwa misingi ya dini
Na ALI HASSAN
Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaaliwa leo hii, siku hii kuu, siku ambayo inasadifu na sherehe za ‘krismasi’ na ‘mwaka mpya’.
Awali ya yote tumshukuru mno wa shukrani Mola wetu Mtukufu kwa kutujaalia kuwa hai na kuwa Waislamu.Ama baada ya kumpongeza, kumshukuru, kumpwekesha na kumsifia sana Allah (SWT), twachukua sawia nafasi hii kumtilia dua na maombi Mtume wetu (SAW), pamoja na aila yake na Maswahaba.
Ewe ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu tunakutana siku hii aula ili kukumbushana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu. Leo hii ndugu yangu muumin wa dini hii ya Kiislamu tunakutana katika kipindi kigumu mno.
Ki vipi?
Kipindi kigumu kutokana na janga hili la maradhi ya Corona. Maradhi ambayo yamegeuza maisha kichwa-ngomba! Ajira zimepotea. Mishahara kukatwa. Ndoa kuvunjika. Asasi kudorora.
Na kila aina ya ugumu wa maisha. Hata hivyo, hatutakiwi sisi waumini-waja kukata tamaa. Ni mitihani kutoka kwa Allah (SWT).Ni kipindi kingine kigumu kwa umma wa Kiislamu sasa hivi tukijiuliza ni kwa vipi jamii yetu, hasa vijana wetu, wanavyokabiliana na ndaro za sherehe hizi za krismasi na mwaka mpya.
Mwanzo, sisi waumini wa dini ya Kiislamu, mara si moja tumeangazia katika ukurasa huu kuhusu asilia, chanzo na maana ya sherehe hizi za krismasi.
Na kwa sasa maimamu, maustadh na mashekhe katika misikiti yetu na majukwaa mbali mbali, wamejikita katika kuangazia nini maana ya sherehe hizi za krismasi.Na ni nini chimbuko la krismasi.Aisha, mara nyingi katika ukurasa huu wetu wa mawaidha, tumeeleza ni lini tunatarajiwa kushereheke mwaka wetu mpya na kwa namna gani.
Sasa hivi katika makiwanda, majukwaa, vyombo vya habari, mitandao na kila pembe ya dunia ni hizo kelele za shangwe za krimasi na mwaka mpya. Vijana wetu wa Kiislamu na umma mzima wa Kiislamu unahitaji kuwa makini sana ili tusije tukaishia kujuta.Tumesema maksudi vijana wetu kwa kuwa sasa hivi wengi wao wamefunga shule na madrassa. Hilo la kwanza.
Pili, wamealikwa katika shamra shamra hizo za krismasi na mwaka mpya. Huko kwenye tafrija hizo ambazo sio za Kiislamu, vijana wetu wasipotahadharishwa na kuonywa mapema, wataishia kula vyakula vya haramu (havikuchinjwa kihalali, mizoga na nyamafu), kunywa mvinyo, kukosa nidhamu na maadili hadi kukiuka miiko ya dini ya Kiislamu.
Matokeo yake je?
Tutasikia visa vya vijana wetu kupigana, kuzini, kutukanana na kujitosa katika kila aina ya uovu, ushirikina, matusi, na kila aina ya uhuni mwingineo.
Sasa hivi ni wasaa mwafaka wa viongozi wa dini kuwasisitizia vijana wetu na umma wetu kujiangalia kwa makini ili wasikiuke mipaka ya dini. Hivi kijana wa Kiislamu unaingiaje katika vilabu, na majumba ya starehe.
Hivi kijana wa Kiislamu utasemaje ukifikwa na majanga yenye kisa na mkasa ukiwa klabuni ati sherehe za krismani na mwaka mpya. Hivi washerehekea nini wewe? Kwa nini sisi Waislamu tusishereherekee siku zetu kuu.
Na twazijua vizuri. Siku yetu kuu ya mwaka mpya twaijua.Inasikitisha sana kuwasikia vijana wetu na hususa ambao wapo katika tasnia ya uanahabari wakiongoza kampeni za krismasi na mwaka mpya. Baadhi ya vijana wetu wakiwa madj kwenye vilabu.
Wengine waandalizi wa sherehe hizi kwa kununua vinywaji, kulipa viingilio, kulipa bendi na kwa njia moja ama nyingine kufaulisha maasia. Hizi si sherehe zetu katu!Ya Rabi tupe salama.Ijumaa Kareem!