Habari Mseto

Aliyeingia Ikulu ‘kuua’ Rais amehepa – Polisi

June 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI 

MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha JKUAT, Brian Bera Kibet ametoroka kutoka Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) alikokuwa amelazwa kupokea matibabu.

Kufuatia ufichuzi huo na wasimamizi wa KNH, hakimu mkuu mahakama ya Milimani, Bw Francis Andayi alimwagiza afisa mkuu wa Polisi eneo la Kilimani (OCPD), Michael Muchiri kuchunguza kisa hicho na kuwasilisha ripoti kortini hapo Julai 3, 2019.

Mahakama ilifahamishwa kuwa mwanafunzi huyo aliyepigwa risasi na maafisa wa wanaolinda Ikulu alikuwa analindwa na maafisa wanne wa polisi kwa zamu.

“Mshukiwa huyo aliyekiri alikuwa anavuka ua wa Ikulu kumuua Rais Kenyatta kwa kumdunga kisu, alikuwa anazuiliwa katika chumba kimoja KNH kupokea matibabu,” Bw Andayi alifahamishwa.

Afisa huyo alieleza mahakama kuwa alipoenda kupokea ripoti jinsi anavyoendelea alifahamishwa kwamba mgonjwa huyo ametoweka.

Mahakama iliambiwa juhudi za kumsaka aliko mshukiwa huyo hazijafanikiwa.

Lakini kulizuka majimbizano makali kati ya mwakilishi wa KNH na afisa anayechunguza kesi hiyo. Bw Andayi alisema lazima hospitali kuu ya KNH na Idara ya Polisi zieleze aliko mshukiwa huyo.

“Mshukiwa akiwekwa chini ya ulinzi wa polisi huwa anachungwa asitoroke. Imekuwaje mshukiwa pamoja na polisi walitoroka KNH,” aliuliza Bw Andayi.

Hakimu alisema mahakama haitakuwa na budi ila kupeleka faili ya kesi hiyo katika mahakama kuu ili maagizo yatolewe yakishurutisha KNH kueleza aliko Bw Kibet. “Tumesikia mara nyingi serikali ikisema itafanya kila juhudi kusaka mshukiwa lakini baadaye taarifa inatolewa kwamba mhusika ameaga,” alisema hakimu.

Afisa huyo wa polisi alikubaliana na hakimu kuwa mmoja akiripotiwa ametoroka mara nyingi hupatikana akiwa amekufa.

Bw Kibet alikiri alipohojiwa na polisi waliomtia nguvuni Ikulu amegadhabishwa na wizi uliokithiri nchini pamoja na ufisadi.