• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 3:55 PM
Aliyekamatwa kwa dai la kuzua hofu ya ugaidi apewa dhamana

Aliyekamatwa kwa dai la kuzua hofu ya ugaidi apewa dhamana

JOSEPH WANGUI na MARY WAMBUI

ALIYEKUWA meneja wa jengo la Doctors Park, Nairobi, ambalo wiki jana lilifanyiwa upekuzi wa kina na wataalamu wa kutegua mabomu, Jumatatu alishtakiwa na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000.

Bi Meera Dinesh Patel alikatamatwa jana asubuhi kwa kushukiwa kuandika kijikaratasi kilichokuwa na maelezo kwamba, bomu lilikuwa limetegwa kwenye jengo hilo lililo eneo la Parklands.

Aliachiliwa baadaye na mahakama ya Milimani jijini Nairobi.

Bi Patel alikana mashtaka kwamba aliandika kijikaratasi hicho kilichopatikana kwenye lango la kuingia ofisi za ghorofa ya tano za jumba hilo.

Wataalamu kutoka Idara ya Makosa ya Jinai (DCI) na Polisi wa Kupambana na Ugaidi(ATPU) ndio walikumbana na kijikaratasi hicho walipokuwa wakifanya ukaguzi.

Kulingana na nakala ya mashtaka, alidaiwa kutenda kosa hilo Januari 30 na kusababisha taharuki miongoni mwa wananchi.

Awali, DCI ilitumia ushahidi ulionaswa kwenye kamera za CCTV ambao uliashiria kwamba, Bi Patel alihusika na ukora huo na kusema alipaswa kuchunguzwa zaidi.

“ Tunatoa onyo kwa mtu yeyote akome kushiriki vitendo vya kutatiza amani au utangamano kwa raia. Watakaoshiriki watachukuliwa hatua kali,” ikasema DCI kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Kwa mujibu wa Idara hiyo, kijikaratasi kilikuwa na maandishi haya, “Kesho ni Ijumaa. Sisi tabomoa Doctors Park yenu. Mimi bado niko kwa building yenu…chungeni Wahindi wote mtachomewa ndani.”

Mshukiwa alidaiwa kukiangusha siku mbili baada ya kustaafu kutoka kwa wadhifa wake akilenga kuteuliwa meneja wa jengo hilo la kibiashara.

“Bi Patel alikuwa ameonyesha nia ya kujaza nafasi ya meneja wa jengo hilo lakini hakufaulu,” ikaongeza taarifa ya DCI.

Hali ya mshikemshike ilitanda jengoni humo wiki jana huku wafanyabiashara waliokodisha vyumba wakilazimika kuondoka na kuwapisha maafisa hao kufanya msako na uchunguzi kubaini iwapo kwa kweli kulikuwa na bomu lililotegwa.

Kisa hicho kilitokea wakati taifa lipo kwenye tahadhari kutokana na uwezekano wa kutokea kwa shambulizi la kigaidi.

You can share this post!

Wazee wapanga kuwapatanisha Ruto na Raila

Mafuriko yazidi kuleta maafa maeneo mbalimbali nchini

adminleo