Habari Mseto

Aliyezuiliwa kwa kuua mwanawe ajiua ndani ya seli

May 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na HILLARY KIMUYU

MWANAMUME ambaye amekuwa akizuiliwa na polisi kwa madai ya kumuua mwanawe wa kambo kwa kumdunga kisu alipoingilia ugomvi baina ya wazazi wake, alijiua mnamo Jumanne.

Dennis Mwema, 18, alijaribu kuingilia kati wazazi wake walipokuwa wakigombana, kabla ya Bw Euticus Githinji kumdunga kisu mara mbili kifuani. Mwathiriwa aliaga baada ya kuvuja damu nyingi nyumbani kwao, mtaa wa Huruma, Nairobi.

Polisi walisema walifahamishwa na wafungwa wengine kuwa Bw Githinji alikuwa amechukua muda mrefu msalani.

“Afisa mmoja aliweza kufungua mlango huo na kumpata akiwa ananing’inia kwa paa la choo akiwa ametumia jaketi lake,” afisa aliyekuwa kwa zamu alieleza.

Polisi walisema walijaribu kwa ushirikiano na wafungwa wengine kumpatia huduma ya kwanza lakini akawa tayari amefariki.

Mapema mwezi huu, mke wa marehemu, Bi Eunice Wanza aliripoti kuwa ugomvi uliishia kwa majonzi baba aliyejawa na hasira alipomdunga kisu mwanawe wa kambo.

Bi Wanza ambaye pia alipata majeraha madogo wakati wa makabiliano hayo, alisema mumewe ambaye wamekuwa pamoja kwa miaka minane, alirudi nyumbani akiwa amelewa na kuanza matusi ambayo yaligeuka kuwa vita.

Wakati wakizozana, mwanas ambaye alikuwa amelala chumbani mwake aliamka na kujaribu kumzuia babake marehemu kumpiga mamake.

Aliongeza kuwa marehemu alimshambulia kwa ngumi na mateke na kumburuta hadi jikoni ambapo alimdunga kwa kutumia kisu cha jikoni.

Mama alijaribu kupata usaidizi kutoka kwa majirani bila kufaulu kwa kuwa alikuwa amewafungia kwa ndani.

Githinji kisha alitoweka alipogundua kuwa amemuua Dennis, lakini alikamatwa wiki moja baadaye.