Habari MsetoSiasa

Anayelengwa katika kesi ya Echesa ni Ruto, mawakili wadai

February 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MAWAKILI wa aliyekuwa waziri wa michezo Rashid Echesa anayekabiliwa kashfa ya Sh40 bilioni ya ununuzi wa silaha za kijeshi walitifua kifumbi kortini Jumatatu huku wakidai anayelengwa katika kesi hiyo ni Naibu Rais William Ruto.

Lakini mahakama iliwaonya mawakili dhidi ya kuropoka mambo yasiyo na ushahidi.

Na wakati huo huo hakimu mwandamizi Bi Kennedy Cheruiyot aliwaachilia Bw Echesa na washukiwa wengine watatu kwa dhamana ya Sh1milioni pesa tasilimu kila mmoja baada ya kulala ndani siku tatu.

Bw Cheruiyot alitupilia mbali ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupinga Echesa, Daniel Otieno Omondi almaarufu Jenerali Juma, Clifford Okoth Onyango almaarufu Paul na Kennedy Oyoo Mboya.

Walipofikishwa kortini jana asubuhi, mawakili Evans Ondieki, Cliff Ombeta na Brian Khaemba mahakama ilifahamishwa kesi dhidi ya Echesa imechochewa kisiasa.

Akipinga Echesa na wenzake wakijibu mashtaka 12 dhidi yao, Bw Ondieki alimweleza hakimu kesi hiyo imechochewa kisiasa na haina “mashiko kisheria.”

Bw Cheruiyot alifahamishwa mwishoni mwa wiki mitandao ya kijamii ilifurika taarifa za wanasiasa watajika wakijadilia suala hilo la Echesa huku wengine wakimtaka Bw Ruto ajiuzulu kwa kuhusishwa na kashfa hiyo ya ununuzi wa silaha za idara ya majeshi.

Hakimu huyo alifahamishwa miongoni mwa waliojadilia kesi hiyo ni pamoja na Gavana wa Kitui Charity Ngilu, Seneta James Orengo na katibu mkuu wa muungano wa vyama vya wafanya kazi Francis Atwoli.

Hakimu alikataa kuwazima watatu hawakujadilia suala hilo katika hafla mbali mbali.

Bw Ondieki alipinga washtakiwa wakisomewa mashtaka 12 dhidi yao kabla ya kesi iliyowasilishwa na DPP katika mahakama iliyoko katika Uwanjani wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kuamuliwa.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi alipinga kusitishwa kwa kesi hiyo akisema “ Polisi wamekamilisha uchunguzi na kuwafungulia washtakiwa mashtaka 12.”

Bw Cheruiyot alitupilia mbali ombi la washtakiwa la kutosomewa mashtaka.