• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
Ardhi ya Ruaraka mnayozozania ni mali ya serikali – Sonko

Ardhi ya Ruaraka mnayozozania ni mali ya serikali – Sonko

Na CHARLES WASONGA

GOVERNOR wa Nairobi Mike Sonko Jumatano alilivalia njuga mjadala tata kuhusu ardhi ambako kumejengwa shule ya msingi ya Drive Inn na Shule ya Upili ya Ruaraka akishikilia kuwa ardhi ya ukubwa wa ekari 13.5 ni mali ya Serikali ya Kitaifa na sio mali ya mtu binafsi kama ilivyoripotiwa.

Kauli ya Gavana Sonko sasa inakinzana na msimamo wa awali wa Wizara ya Ardhi na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kwamba ardhi hiyo ni mali ya mtu binafsi.

Asasi hizo mbili zilikuwa zimesema kuwa utaratibu uliofaa ulifuatwa katika kumlipa fidia Bw Francis Mburu ambaye alidaiwa kuwa mmiliki wa kipande hicho cha ardhi.

Alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu na Uwekezaji (CPAIC) ili kutoa mwanga kuhusu umiliki wa ardhi hiyo, Gavana Sonko alisema stakabadhi zilizoko katika City Hall za mwaka wa 1982 zinaonyesha kuwa ardhi hiyo ni ya Serikali.

Inadaiwa kuwa Bw Mburu na maafisa wa NLC walivunja sheria kuhusiana na suala zima la umiliki wa ardhi hiyo kwa niaba ya Shule ya Upili ya Ruaraka na ile ya Msingi ya Drive Inn

Wapelelezi wanachunguza ikiwa kampuni kwa jina Afrison Import Export Ltd na Hueland Ltd zinazomilikiwa na Mburu na maafisa kutoka Wizara za Fedha na Elimu pamoja na tume ya NLC walishiriki njama ya kulipa ridhaa kwa kampuni hiyo (Afrison) kwa ardhi ambayo ilikuwa imewasilishwa kwa serikali kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Uchunguzi ulioendeshwa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ardhi ulionyesha kuwa NLC ilianzisha mchakato wa ununuzi wa kipande hicho cha ardhi kwa Sh3.3 bilioni baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa wakurugenzi wa kampuni ya Afrison.

Wapelelezi wanaamini kuwa NLC ililipa Afrison Sh1.5 bilioni, kama malipo ya awali, kinyume cha sheria, kwa sababu ukweli ni kwamba shule hizo zilijengwa katika ardhi ya serikali. Wanasema maafisa wakuu wa serikali walihusika katika sakata hiyo ambapo serikali ililipia ardhi ambayo ni mali yake.

Sh1.7 bilioni hazijalipwa mpaka sasa baada ya mpango huo kuibua pingamizi.

“Jinsi nijuavyo, ardhi hiyo haikupasa kulipiwa fidia ilipotumika kujenga shule hizo mbili kwa sababu ni mali ya serikali kuu,” Sonko akaambia wanachama wa CPAIC wakiongozwa na Seneta wa Kiambu Kimani wa Matang’i.

Sonko aliwaambia maseneta kuwa ugawaji wa ardhi ya ukubwa wa ekari 96 inayojumuisha ardhi kulikojengwa makao makuu ya GSU ulifanywa Septemba mnamo 1982.

Aliwasilisha stakabadhi, zikiwemo ramani, na kumbukumbu ya mikutano iliyoandaliwa chini ya iliyokuwa Tume ya Jiji la Nairobi kuthibitisha kuwa ardhi hiyo iligawanywa.

“Ardhi yote ya ukubwa wa ekari 96, ikiwemo ekari 37 inayokaliwa na makao makuu ya GSU, ekari 13.5 kulikojengwa shule ya upili ya Ruaraka na ile ya Msingi ya Drive Inn ilikuwa mali ya umma. Hii inajumuisha ekari 59 iliyochukuliwa na Halmashauri ya Barabara za Mjini (KURA) kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya outering, kambi ya chifu na sehemu nyingine ikatwaliwa na wanyakuzi,” akasema Bw Sonko.

Gavana Sonko aliiambia kamati hiyo kwamba kuna genge la maafisa City Hall ambayo wamekuwa wakinyakua ardhi za watu na kuuzia wanunuzi wasio na habari.

“Tangu nilipoingia afisini, nimewasimamisha kazi maafisa kadha wa ardhi ambao wamekuwa wakishirikiriki njama kama hii ya unyakuzi wa ardhi. Itakuwa kuwa mapema mwaka jana, nusra tupigane na mtangulizi wangu katika kamati hii nilipoubua suala la unyakuzi wa ardhi ya Mkenya fulani wa asili ya Kihindi katika mtaa mmoja kando la barabara ya Ngong’,” akasema.

Gavana huyo alisema afisi yake hupokea malalamishi mengine kuhusu masuala ya ardhi, akisema maafisa wake wamekuwa wakifanya kila wawezalo kuhakikisha kuwa wakazi wa Nairobi wanasaidiwa.

Mwezi jana, Waziri wa Ardhi Farida Karoney alifika mbele ya kamati hiyo ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma na kusisitiza kuwa ardhi hiyo ya Ruaraka ni mali ya kampuni za Afrison Export Import na Hueland Ltd.

You can share this post!

‘Bora Uhai’ ni msemo wa kiutumwa, afafanua...

HAKUNA KUPUMUA: Gharama ya maisha kuzidi kupanda

adminleo