Habari Mseto

Mwanamume mwenye bashasha amuua mkewe

November 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MERCY KOSKEY

SIMANZI imekumba mtaa wa Free Area mjini Nakuru baada ya mwanamume mmoja kudaiwa kumnyonga mkewe hadi kufa hapo Jumapili.

Maafisa wa polisi sasa wanamtafuta mshukiwa huyo aliyetoweka baada ya kutenda unyama huo.

Mwili wa marehemu Naomi Wanjiru mwenye umri wa miaka 35, ulipatikana kwenye chumba chake cha kulala huku mwanawe akiwa kitandani.

Mwanawe huyo ameambia Taifa Leo Dijitali kuwa aliiingia kwenye chumba cha mama yake ili apate kujua kwa nini amelala kwa muda mrefu lakini alipojaribu kumwamsha, hakuitika.

“Mama alikawia kuamka, hivyo nikashikwa na wasiwasi mkubwa kwani si kawaida yake kulala hasa siku ya Jumapili. Nilipojaribu kumwamsha hakuitika, hivyo nikaenda kuwaita majirani,” alisema mtoto huyo.

Mwili wa mwendazake ukiondolewa na majirani. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na kijana huyo mwenye umri wa miaka kumi na saba, Titus Kingori, mshukiwa alikua baba wa kambo na walikua wamekaa pamoja kwa zaidi ya miaka tano na hajawahi kugombana na wao.

“Mimi na ndugu zangu watatu tumemjua mshukiwa kama baba yetu kutoka mwaka wa 2015. Tumekuwa tukiishi pamoja kama familia. Nashangaa kwa nini alifanya kitendo hiki,” alisema.

Kulingana na kamanda wa polisi wa Kaunti ndogo ya Nakuru Mashariki Ellena Kabukuru, walipokea habari ya mauaji kutoka kwa chifu wa eneo hilo na kufika kwenye eneo la tukio.

Aliongeza kuwa polisi wako macho kumtafuta mshukiwa na punde atakapokamatwa atafikishwa kortini ili uchuguzi ufanywe.

“Tumeanzisha uchuguzi wetu kuhusu mauaji haya na polisi wako macho kumtafuta. Tukimkamata mshukiwa atafikishwa kortini,” alisema Bi Kabukuru.

Majirani walimshangaa mshukiwa huyo kutenda unyama huo. Picha/ Richard Maosi

Kulingana na Bi Kabukuru, mwili wa mwendazake haukuwa na majeraha mwilini na hivyo inashukiwa kuwa alinyongwa na mumewe kabla ya kutoweka.

Majirani walisema kuwa wameishi pamoja na mwendazake kwa muda mrefu na hakuwahi kuonyesha dalili zozote za matatizo ya kinyumbani kwani alikua mtu mwenye furaha.

Jirani huyo alisema kuwa aliamshwa na kamsa ya mtoto huyo alipokuwa anaomba usaidizi kutoka kwa majirani.

“Tulipigwa na butwaa tulipoingia chumbani na kumkuta amefariki. Tumepoteza jirani mzuri sana alikua mtu wa bidii sana,” alisema jirani huyo.