Habari Mseto

Ashtakiwa kutumia kisingizio cha msiba kuomba mbunge pesa

October 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

MKAZI wa Kaunti ya Kakamega, Erastus Matende Omwoma ameshtakiwa kwa kumlaghai Mbunge wa Lurambi Titus Khamula Mukhwana Sh46,000 akimdanganya watu wa familia yake wamekufa.

Akiwa ameinamisha uso kwa haya na kujaribu kuwakwepa wapigapicha za magazetini, televisheni na mitandao mbalimbali, Matende alikana alimlaghai Bw Mukhwana kitita hicho cha pesa alichodai ni za kuwasaidia waliokuwa na makiwa.

Matende mwenye umri wa miaka 28, alifikishwa mbele ya hakimu mkuuwa  mahakama ya Milimani, Nairobi Bi Martha Mutuku na kukanusha shtaka la kumtapeli mtunga sheria huyo.

Bi Mutuku alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka Bw Anderson Gikunda kwamba mshtakiwa alipokea pesa hizo katika afisi za Wabunge katika jengo la Continental Nairobi.

Matende aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana akisema “hawezi kupata dhamana ya kiwango cha juu kwa vile hana kazi maalum.”

Akasema: “Mimi hufanya kazi za kibarua huku na kule na sina pesa za kulipa dhamana. Naomba niruhusiwe kutia saini stakabadhi ya mahakama kwamba nitafika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi,” Matende alimsihi hakimu.

Kiongozi wa mashtaka hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana ila alimsihi hakimu azingatie mshtakiwa alitumia uwongo kupokea pesa kutoka kwa mbunge huyo.

Hakimu alimwachilia Matende kwa dhamana ya Sh50,000 na kuamuru kesi isikizwe Novemba.