Askofu akamatwa kuhusiana na mauaji ya Matungu
Na SHABAN MAKOKHA
KIONGOZI wa kidini amekamatwa kuhusiana na mauaji yanayotekelezwa na genge katika eneobunge la Matungu, Kaunti ya Kakamega. Kufikia sasa watu 14 wameuawa na genge hilo katika muda wa miezi miwili iliyopita, kwenye mauaji ambayo polisi wanasema ni ya kisiasa.
Askofu Nanjira Makokha wa Kanisa la Christian Warrior Prayer Ministries, alikamatwa Ijumaa na kikosi cha maafisa wa GSU ambao walivamia nyumbani kwake katika kijiji cha Lung’anyiro.
Polisi walisema mhubiri huyo alikamatwa baada ya simu yake kuhusishwa na msururu wa habari za kutisha zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii.
OCPD wa Matungu, John Matsili alithibitisha kukamatwa kwa askofu huyo, akisema anaendelea kuhojiwa.
“Tukipata anahusika atafikishwa kortini kwa kuchapisha habari za kutisha katika kundi la Whatsapp,” Bw Matsili akasema.
Mkewe mhubiri huyo, Nancy Kibisu alisema mumewe alikamatwa saa mbili usiku na maafisa wa polisi waliotumia magari matano.
“Tulikuwa tukitazama televisheni na mume wangu wakati polisi walipofika na kumkamata mhubiri huyo,” akasema.
Alisema maafisa wa GSU waliokuwa wamejihami walitoka kwenye magari na kuzunguka boma zima, wakielekeza bunduki zao katika nyumba.
“Aliwasalimu lakini wakamwamrisha ainue mikono kama ishara ya kujisalimisha. Alitii maagizo na maafisa watano wakamwendea na kumkamata. Aliuliza sababu yao kumfanyia hivyo na afisa mmoja akamzaba kofi,” Bi Kibisu akasema.
Mhubiri huyo aliwaelekeza maafisa hao ndani ya nyumba, ambapo wanasemekana kufanya msako na kuhangaisha waliokuwa mle nyumbani wakiwemo watoto.
“Walikuwa wakituambia tutoe bunduki walizodai mume wangu amekuwa akiwapa vijana kufanya uhalifu usiku. Tuliwaambia hatuna bunduki yoyote na kuwa hatukuelewa walichokuwa wakisema. Walinipiga kofi na kumsukuma mtoto wangu mkubwa, wakituambia tuache kucheza nao na tuwape bunduki, pingu na sare za polisi,” akaeleza.
Bi Kibisu alisema maafisa hao walichukua laptopu, simu nne, kitabu cha wageni kujisajili na cheti cha usajili wa kanisa.
Kulingana naye, mmoja wa maafisa hao alidai walikuwa na habari kuwa kanisa hilo, ambalo liko nje ya nyumba yao, lilikuwa likitumiwa kutekeleza maovu.
Polisi wamewakamata watu 16 kuhusiana na mauaji hayo. Washukiwa wawili waliuawa kwa kupigwa risasi, huku watano wengine wakipigwa mawe na raia.