Askofu akamatwa waumini wakitoroka Mikindani
Na WINNIE ATIENO
POLISI katika eneobunge la Jomvu wamewatia mbaroni askofu na mhubiri wake waliokuwa mstari wa mbele wakiongoza misa ya Jumapili katika kanisa la Healing and Restoration lililopo Mikindani.
Wakati wa operesheni hiyo, zaidi ya waumini 20 wamekwepa mtego wa polisi.
Machi 2020 Rais Uhuru Kenyatta alipiga marufuku mikutano yote ya hadhara katika maeneo ya kuabudu ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Afisa mkuu wa eneo la Jomvu Bw James Mutua amesema wamepata fununu kuhusu maombi yaliyokuwa yakifanyika katika kanisa hilo licha ya marufuku yaliyotangazwa na serikali.
“Tumempata askofu huyo akiongoza sala na mhubiri wake, lakini waumini wakatoroka walipotuona. Wawili hao watashtakiwa Jumatatu kwa kukiuka agizo la serikali dhidi ya marufuku ya maeneo ya ibada,” amesema Bw Mutua huku akiwaonya viongozi wa kidini na waumini dhidi ya kuvunja sheria na kanuni.
Bw Mutua amesema polisi wataendelea kuimarisha usalama na kushika doria ili kuhakikisha wakazi wanaheshimu maagizo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa kidini na waumini wao wamekuwa wakikiuka agizo la Wizara ya Afya dhidi ya mikutano ya hadhara huku wakiendelea kufanya maombi kanisani.
Wairai serikali
Haya yanajiri majuma kadhaa baada ya baadhi ya viongozi wa kidini, Waislamu kwa Wakristo, kuisihi serikali iruhusu kufunguliwa kwa maabadi ili waumini wafanye ibada.
Aidha walisisitiza kuwa wangefuata maagizo ya Wizara ya Afya ili kuepuka virusi hivyo hatari.
Makanisa kadhaa yanaendeleza mahubiri au injili kupitia mitandao ya kijamii baada ya serikali kupiga marufuku ibada kwenye sehemu za kuabudu.