Askofu asihi maombi kwa wapatanishi
GITONGA MARETE Na JOSEPH WANGUI
MMOJA wa watu 14 waliochaguliwa kusimamia juhudi za kupatanisha taifa amesihi Wakenya wawaombee kwani majukumu waliyopewa ni mazito.
Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga walichagua kamati hiyo baada ya kuafikiana Machi 9 ili kuleta umoja baada ya mgawanyiko uliosababishwa na siasa za uchaguzi wa mwaka uliopita.
Akihutubu wakati wa harambee ya ujenzi katika Kanisa la Kaaga Methodist, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist nchini, Lawi Imathiu, alisema kazi ya kamati hiyo ni kushirikiana na viongozi wote na Wakenya ili kutimiza umoja wa taifa.
“Tutajitahidi na kujitolea katika jukumu hili lakini inafaa pia nyinyi mjitolee kwani hatuwezi kufanikiwa peke yetu. Hii si kazi rahisi na majukumu tuliyopewa yanahitaji maombi mengi na uungwaji mkono. Tukishindwa, sote 14 tutalaumiwa,” akasema.
Aliongeza kuwa endapo watashindwa, Wakenya pia watafaa kulaumiwa kwani ni jukumu lao kuhakikisha kamati inatenda kazi zake ipasavyo.
“Mkiona hatufuati njia inayofaa, msinyamaze. Kuweni huru kutuambia tunapokosea,” akasema.
Aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kiambu, Bi Anne Nyokabi, ambaye alikuwa mgeni mkuu katika hafla hiyo alisema Rais Kenyatta na Bw Odinga walionyesha kuwa nchi ni muhimu kuwaliko walipojitolea kushirikiana.
“Salamu yao ilikuwa muhimu kwa sababu ni wito wa kuboresha nchi yetu,” akasema. Bi Nyokabi.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Jubilee, Bw Raphael Tuju, alitoa wito kwa wanasiasa kuunga mkono muafaka wa upatanisho.
Bw Tuju, ambaye pia ni waziri alisema chama hicho kinaunga mkono muafaka wa viongozi hao wawili lakini akakiri haujaeleweka vyema kwa wanasiasa.
“Rais alijitokeza akahakikishia kila mmoja kuwa muafaka ni kwa manufaa ya nchi na kupunguza taharuki. Hakuna mtu anafaa kuhisi kwamba atadhulumiwa na muafaka huu. Ni kwa manufaa ya nchi na wanasiasa wote kutoka pembe zote za nchi,” akasema Bw Tuju.
Alizungumza baada ya kuhudhuria mkutano wa uongozi wa Chama cha Jubilee katika Hoteli ya Sportsman Arms iliyo Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.
Alisema mkutano huo ulinuia kuamua mwelekeo ambao chama kitachukua kufuatia ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Kuhusu wito wa marekebisho ya katiba, Bw Tuju alisema Jubilee hakipatii uzito suala hilo lakini kimejitolea kutimiza malengo ya manifesto yake.
Hata hivyo, aliongeza kuwa kila Mkenya ana haki ya kupendekeza kile anachotaka na Jubilee itaheshimu matakwa ya Wakenya.