Askofu aunga mkono wito wa kudhibiti makanisa
Na OSBORNE MANYENGO
ASKOFU wa Kanisa la Anglikana (ACK) Dayosisi ya Kitale, Dkt Emmanuel Chemengich ameunga mkono juhudi za kudhibiti makanisa nchini.
Akiongea na wanahabari katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Bishop Muge, Kaunti ya Trans Nzoia, Askofu Chemengich alisema hatua hiyo itasaidia kuzima baadhi ya viongozi wa makanisa wanaopuja waumini wao kwa manufaa yao ya kibinafsi.
Alisema kuna makanisa mengi ambayo yamebuniwa nchini kwa lengo la kuwapunja waumini wakitumia neno la Mungu kinyume na mafunzo ya kidini.
Alisema wahubiri ambao wametapeli waumini wanafaa kukabiliwa vikali kisheria.
Askofu Chemengich pia aliunga mkono vita dhidi ya ufisadi, lakini akasema havifai kufanywa kwa njia ya ubaguzi, huku akipendekeza mafunzo ya maadili yaanze kufunza kwa wanafunzi shuleni.
Akiunga mkono wito wa Askofu Chemengich kuhusu ufisadi, Mbunge wa Endebess, Dkt Robert Pukose alisema kuwa ufisadi ni ugonjwa mbaya kwa Kenya.
“Mimi ni mmoja wa wale ambao wanaunga mkono wito wa Rais wa kumaliza ufisadi nchini. Lakini njia ambayo tume husika zinafanya kazi, mimi sikubaliani nayo kabisa, maana siasa imeingia ndani kutumika kuwafungia wengine kuwania vyeo fulani 2022,” akasema Dkt Pukose.