Atwoli ataka mabadiliko ya mawaziri, aishutumu EACC
VICTOR OTIENO na KALUME KAZUNGU
KATIBU Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli amemwomba Rais Uhuru Kenyatta kufanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri huku akishutumu vikali Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kwa kufeli katika vita dhidi ya ufisadi.
Bw Atwoli amedai kwamba mabadiliko hayo yataimarisha huduma zinazotolewa na serikali na pia kujumuisha wandani wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga serikalini kama njia ya kutimiza mwafaka kati ya Rais na Bw Odinga.
Akizingumza mjini Kisumu, Bw Atwoli alisema kwamba salamu za maridhiano kati ya viongozi hao wakuu mnamo Machi 9 imesaidia kurejesha amani na utulivu nchini na baraza la mawaziri linalojumuisha pande zote litazidisha mshikamano na umoja.
“Ningependa kumshukuru kiongozi wa upinzani nchini kwa kukubali kufanya kazi na Rais kwa sababu hatua hiyo imemaliza taharuki iliyokuwa ikishuhudiwa. Hata hivyo, lazima pawepo mabadiliko ya baraza la mawaziri ili tusonge mbele. Namwomba Rais atekeleze hayo haraka ili jamii ambazo hazijawakilishwa serikalini zipate nafasi,” akasema Bw Atwoli.
Bw Atwoli ambaye alikuwa akizungumza jana wakati wa mafunzo yaliyowaleta pamaoja maafisa wa muungano wa leba kutoka barani Afrika alimtaka Rais Kenyatta aandae mkutano na mawaziri wake ili awaeleze ajenda walizonazo na Bw Odinga kufuatia mwafaka wa Machi 9 ili waweze kuzitekeleza.
“Natarajia kila waziri aunge mkono handshake na ningemwomba Rais Kenyatta akutane na mawaziri na awafafanulie kila ajenda ili wawe katika mstari wa mbele kuzitekeleza,” akaongeza katibu huyo mkuu wa COTU.
Aidha, kiongozi huyo alishutumu vikali tume ya EACC kwa kushindwa kukabiliana na ufisadi na kuachia taasisi nyingine kazi hiyo ingawa maafisa wake kuendelea kupokea ufadhili mkubwa kutoka kwa serikali.
“Ningependa kuwaambia EACC waachane na vita dhidi ya ufisadi kwa sababu nilitoa taarifa kuhusu wizi wa Sh8 bilioni za NSSF mwaka wa 2013 lakini hawajawahi kufanya uchunguzi hadi leo. Wanalalamika kuwa majukumu yao yanatekelezwa na watu wengine ilhali wameshindwa na kazi,” akasema Bw Atwoli akirejelea sakata ya uuzaji nyumba katika mtaa wa Tasia jijini Nairobi.
Vilevile, alitaka mgao wa fedha usitolewe kwa EACC na badala yake fedha hizo zielekezwe kwa idara ya upelelezi (DCI) na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma(DPP).
Kwingineko, Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Utangamano imeahidi kuandaa ripoti itakayohakikisha wakazi wa miji ya mpakani mwa Lamu na Somalia wanapokea huduma za serikali sawia na Wakenya wengine.
Wakazi wa vijiji vya Kiunga, Ishakani, Madina, Basuba, Mkokoni, Kiwayu, Ndau na sehemu nyingine za mpakani wamekuwa wakiilaumu serikali kwa kuwabagua katika utoaji wa huduma muhimu za serikali.
Miongoni mwa huduma hizo ni utoaji wa vitambulisho, pasipoti za kusafiria, ukosefu wa huduma bora za afya, elimu na vijana kubaguliwa katika ajira za serikali.
Wakizungumza walipokutana na wakazi mjini Lamu, Jumatatu, wanachama wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ruweida Obbo, walisema ni haki ya kila Mkenya kupewa huduma za serikali bila kubaguliwa eneo analoishi, kabila, dini au rangi.
Bi Obbo aliwaahidi wakazi hasa wale wa mpakani mabadiliko hivi karibuni punde kamati hiyo itakapoandaa na kuwasilisha ripoti yake bungeni baada ya kupokea maoni ya wananchi.
“Tumesikia kilio cha wakazi wa hapa. Mimi binafsi natoka Kiunga na ninakubaliana na wananchi wangu kwamba eneo hilo limetengwa na kutelekezwa kwa muda mrefu.
Kama kamati ya utangamano, tutahakikisha vilio vyote ambavyo tumepokea kutoka kwa wananchi vinanakiliwa kwenye ripoti yetu kabla ya kuiwasilisha bungeni. Mtarajie mabadilikio makubwa katika utoaji wa huduma za serikali siku zijazo,” akasema Bi Obbo.
Naye Mbunge wa Matuga, Kassim Tandaza, ambaye pia ni mwanachama wa kamati hiyo, alisema uwiano na utangamano wa kitaifa na majimbo katu hauwezi kuafikiwa ikiwa baadhi ya maeneo hapa nchini yanabaguliwa katika utoaji wa huduma za serikali.
Bw Tandaza alisema kamati hiyo itawajibika ipasavyo ili kuona kwamba matatizo hasa ya watu wanaoishi kwenye sehemu za mpakani, ikiwemo utoaji wa vitambulisho, ajira kwa vijana na masuala mengine ya kimsingi yanashughulikiwa.
Alisema ni haki ya kila mkenya kupewa huduma mahali alipo.