Habari Mseto

Aukot adai Mswada wa Punguza Mizigo uliyumbishwa na wanasiasa wenye tamaa

October 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KIONGOZI wa Thirdway Alliance Dkt Ekuru Aukot amesema kuanguka kwa Mswada wa Punguza Mizigo kumechangiwa zaidi na wanasiasa wenye tamaa na ubinafsi.

Dkt Aukot pia amesema ifahamike wazi kuwa si wananchi walioangusha mswada huo ambao siku yake ya kujadiliwa na kupitishwa na mabunge ya kaunti ilifikia nanga jana, Oktoba 15.

Kufikia muda uliowekewa, ni bunge moja tu, Uasin Gishu, lililokuwa limeupitisha. Mabunge yapatayo 18 yakiwemo Garissa, Nakuru, Nyamira, Nyeri, Homa Bay, Nairobi, Kirinyaga, Makueni, Siaya na Murang’a yaliukataa.

Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen Jumanne usiku, Dkt Aukot alisema viongozi na wanasiasa wenye ubinafsi walifanya kampeni ya kuangusha mswada huo kwa sababu ni “mvulana” aliyetoka jamii ndogo na isiyo na ushawishi mkubwa serikalini.

“Mswada wa Punguza Mizigo umeangushwa na wanasiasa ila si wananchi. Kwa mfano, muungano wa Nasa ulijitokeza na kueleza bayana utauangusha. Ulianguka kwa sababu ya viongozi na wanasiasa wenye tamaa na ubinafsi,” akasema kiongozi huyo kutoka jamii ya Turkana.

National Super Alliance ni muungano unaojumuisha chama cha ODM, Wiper, Ford Kenya na ANC. Ingawa Katibu Mkuu wa ODM akihojiwa na chombo kimoja cha kimataifa aliwahi kukiri “ni kama umekufa.”

Viongozi wa vyama hivyo wamekuwa katika mstari wa mbele kucharura mswada huo, wakihoji pendekezo la kupunguza nafasi za viongozi bungeni na katika kaunti unapania kufungia jinsia moja nje na hata baadhi ya jamii.

Kiongozi wa ODM amenukuliwa akikejeli Punguza Mizigo kama “Punguza Punda”, na kushawishi mabunge ya kaunti na Wakenya yasiukubaliwe kwa kuwa hautatui shida za wananchi.

Waziri huyo Mkuu wa zamani anahimiza taifa kusubiri ripoti ya jopokazi la BBI lililoteuliwa naye pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kupitia salamu za heri maarufu kama ‘Handisheki’ za hapo Machi 9, 2018.

Dkt Aukot hata hivyo jana alisema amekuwa akijaribu juu chini kutaka kujua kwa nini Bw Raila anapigia debe kuangusha mswada huo. “Nimekuwa nikiuliza kiongozi huyo wa ODM kwa nini anataka Punguza Mizigo ianguke,” akasema.

Ili kuupitisha, mswada huo ulihitaji uungwaji mkono na zaidi ya kaunti 24. Iwapo ungepitishwa, ungewasilishwa katika bunge la kitaifa na lile la seneti.

Mswada huo unapendekeza kubadilisha baadhi ya vipengele vya Katiba ya sasa, iliyoidhinishwa 2010, kwa mujibu wa Kifungu cha 257 cha Katiba hiyo.

Kulingana na tovuti ya Thirdway Alliance, Mswada huo unalenga kupunguza nyadhifa za kisiasa ambazo Dkt Aukot anadai zinachangia kuongezeka kwa matumizi ya raslimali za serikalini.

Kwa mfano, Punguza Mizigo inapendekeza viti vya wabunge vipunguzwe kutoka 416 hadi 147.

Pia, awamu mbili za miaka mitano kila moja za utawala utawala wa rais zifanywe awamu moja ya miaka saba. Katika pendekezo hilo, rais anapaswa kulipwa Sh500, 000 kwa mwezi ambapo kwa sasa mshahara wadhifa huo ni Sh1.4 milioni.

Mshahara wa mbunge kwa mujibu wa mswada huo unapaswa kuwa Sh300,000 huku marupurupu wanayopokea yakiondolewa. Mswada huo unapendekeza matumizi ya shughuli za bunge la kitaifa kupunguzwa kutoka Sh36.8 bilioni hadi Sh5 bilioni, Dkt Aukot akieleza kwamba hatua hiyo itaondolea walipa ushuru kima cha Sh31.8 kwa mwaka.

Punguza Mizigo pia inapendekeza kesi za ufisadi zisikilizwe na kuamuliwa kwa muda wa siku 30, na rufaa siku 15.

Dkt Aukot Jumatatu alisema Thirdway Alliance hivi karibuni itatoa mwelekeo licha ya Mswada huo kurambishwa sakafu.

Mnamo Jumatano, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) hadi mtaani Westlands, Rais Kenyatta alihimiza wananchi kusubiri ripoti ya pamoja ya jopokazi la BBI, ambalo limekusanya maoni na mapendekezo ya Wakenya kutoka sehemu mbalimbali za nchi.

Kauli hiyo pia aliiradidi akiwa eneo la Ngong wakati wa uzinduzi wa uchukuzi na usafiri reli ya SGR kati ya Nairobi na Naivasha. Kiongozi huyo wa taifa alisema BBI inapania kuunganisha Wakenya, kuzika ukabila na uhasama unaoibuka kila mwaka wa uchaguzi mkuu Kenya.