Azimio ni nyumbani, hatubanduki ng’o, viongozi wa Wiper wasema
KUNDI la viongozi waliochaguliwa katika Chama cha Wiper wamesema hawabanduki Azimio huku wakithibitisha kuwepo migawanyiko katika muungano huo kuhusiana na azma ya kujiunga na serikali ya Rais William Ruto.
Wakihutubia vyombo vya habari Jumanne, wabunge na maseneta wa chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka, walisisitiza kuwa Azimio iko imara na kwamba maamuzi ya watu binafsi hayatatikisa muungano huo.
Viongozi hao wanaojumuisha Seneta wa Kaunti ya Makueni, Dan Maanzo, Seneta Mteule Kaunti ya Lamu, Shakila Mohamed, na Mbunge wa Matungulu, Stephen Mule, walisema kuna watu binafsi waliopania kutawanya Azimio tangu Rais Ruto alipotangaza azma ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.
Walitoa onyo kwa baadhi ya viongozi katika vyama tanzu wanaodai wamekuwa wakimsuta kinara wa Wiper kwa kukataa wito wa kujiunga na serikali ya Dkt Ruto huku wakisema vyama tanzu sasa vitakuwa vikipigwa msasa kabla ya kujumuishwa katika Azimio.
“Azimio iko imara. Tunajua kuna watu wamekuwa wakijitahidi juu chini kusababisha migawanyiko na kuchukua hatua za ghafla katika Azimio,” alisema Bw Mule.
Kulingana na mbunge wa Matungulu, kulikuwa na juhudi za kushawishi Wiper ijiunge na serikali lakini, “tulikataa. Hatuwataki.”
Alisema kuna njama za kuigawanya Azimio ili kuwanyima haki Wakenya wanaowasilisha kilio chao kupitia maandamano yanayoongozwa na vijana wanarika almaarufu kama Gen Z.
“Yeyote anayetaka kuvuka kambi acha afanye hivyo kwa kutumia tiketi yake na wala si kwa kutumia tiketi ya chama wala muungano.”
Haya yanajiri wakati ambapo upinzani umeonekana kugawanyika vibaya huku kinara wa ODM, Raila Odinga akikabiliwa na kitendawili kigumu hasa kuhusu wandani wake wanaomezea mate nyadhifa katika baraza jipya la mawaziri wa Kenya Kwanza.
“Wanaotaka kujiunga na Baraza jipya wako huru kufanya hivyo. Kwa wanaotaka kuteuliwa ni sawa watapigwa msasa,” alisema Seneta Maanzo.
Huku wakiapa kwamba hawataunga mkono “serikali inayozama” viongozi hao wa Wiper wamesisitiza kuwa watasimama pamoja na Wakenya kutetea mabadiliko kutoka kwa serikali ya Kenya Kwanza kabla ya Uchaguzi Mkuu 2027.
“Vijana hawatasitisha maandamano hadi haki na matakwa yao yatakapotimizwa. Tunawahimiza Wakenya kuandamana kwa amani na tutatetea haki ya Wakenya,” alisema Bw Mule.
Seneta wa Lamu alimpongeza Bw Odinga kwa kukataa kujiunga na serikali akisema,”Wale wanataka kuhama, acha wahame bila kuvuta Azimio. Kiongozi wetu Kalonzo Musyoka asihangaishwe.”