Habari Mseto

Baa zote zafungwa kulazimisha vijana kuoa

April 8th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA PETER MBURU

Viongozi wa usalama kutoka eneo la Koibatek, Baringo wamefunga baa zote pamoja na maduka mengine ya kuuzia pombe, baada ya unywaji wa pombe haramu kuzuia zaidi ya vijana 400 kuoa.

Suala la vijana wa eneo hilo kukosa kuoa liliangaziwa na Taifa Leo miezi michache iliyopita, hali ambayo ilikuwa imewasukumia wazee katika jamii kuchukua majukumu ya ulezi wa wajukuu wao, baada ya ulevi kuadhiri sehemu kubwa ya jamii.

Kufuatia mikutano mingi ya wanajamii wa eneo hilo, wakazi walifikia uamuzi kuwa suluhu ya uozo uliokita katika jamii ingepatikana tu endapo uuzaji wa pombe ungeharamishwa.

Kulingana na viongozi wa eneo hilo, unywaji pombe kupita kiasi umepelekea hasara nyingi, zikiwemo vijana wa umri mdogo kufariki, ndoa kuvunjika, wazazi kutelekeza majukumu ya ulezi wa wanao na zaidi ya yote vijana 500 wakikosa kuoa kutokana na adhari zake.

Wakazi wasikiza viongozi wao eneo la Koibatek kwenye kikao kilichokubaliana kuwa mabaa, vilabu na maduka mengine yote ya kuuza pombe yafungwe ndani ya siku saba. Picha/ Peter Mburu

“Vijana wamekataa kuoa na kuanza familia kwa kuwa vinywaji wanavyobugia vimewanyima nguvu za uzazi. Vijana sasa wanaingiliana kimwili na wanawake wa vilabuni ambapo wengi wamepata magonjwa hatari kama UKIMWI,” wakasema wakazi wa eneo hilo kwenye barua waliyomwandikia mwenyekiti wa kupeana leseni kwa wauza pombe eneobunge la Eldama Ravine.

Wakazi aidha walilalamika kuwa kunaibuka pengo baina ya kizazi cha vijana wa sasa ambao licha ya kutooa, wachache wanaooa wanashuhudia uvunjikaji mkubwa wa ndoa zao kutokana na ulevi kuadhiri masuala ya familia.

“Maboma mengi sasa yanaongozwa na kina mama kutokana na ulevi wa mabwana, huku katika visa vingine watoto wakitekelezwa na wazazi wote na mzigo wa majukumu kulazimishwa kuangukia mababu na nyanya zao,” wakazi wakasema.

Kwenye barua ya pamoja iliyotokana na kikao cha wakazi na viongozi wa eneo hilo Machi 12, wakazi waliitaka bodi ya kutoa leseni kwa uuzaji wa pombe kuharamisha maduka yote ya kuuza pombe katika maeneo ya Timboroa, Seguton na mengine ya Koibatek yaliyoadhirika vikubwa na ulevi wa pombe hizo ndani ya kipindi cha wiki moja.

Viongozi wa Koibatek wakiwa katika kikao kilichofikia uamuzi mabaa, vilabu na maduka mengine yote ya kuuza pombe yafungwe ndani ya siku saba. Picha/ Peter Mburu

Baadhi ya wazee waliozungumza na Taifa Leo walisema kuwa ulevi huo sasa umekita mizizi na kukiuka kanuni na itikadi, wakihofia hatari ya vizazi vyao kuangamia.

“Takriban kila boma eneo hili lina kijana ama wawili waliofikisha umri wa kuoa lakini bado hawajafanya hivyo, wala kuonyesha dalili za kufanya hivyo. Wengi wao hata hawana wapenzi na wachache walio nao ni wale wazee wa vilabuni,” akasema mzee James Kariuki.

Chifu wa kata ya Timboroa Bw Jacob Njehia naye alieleza Taifa Leo kuwa ulevi ulipelekea vijana kutofanya kazio na kushinda vilabuni, huku kukishuhudiwa ongezeko la utovu wa usalama.

Wamiliki wa vilabu sasa wamepewa chini ya wiki moja kufunga maduka yote ya kuuza pombe, katika hatua inayonuiwa kutakaza eneo hilo na kurejesha urazini wa kizazi kinachoelekea kuangamia.