Habari Mseto

Baba katili kula madondo jela kwa kunajisi na kulawiti wanawe

Na KASSIM ADINASI June 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MNAMO Juni 16, 2022 msichana mwenye umri wa miaka 14 katika Kaunti ya Siaya alimshangaza mwalimu wake alipofichua kuwa babake amekuwa akimbaka mara kadhaa.

Mwalimu huyo alimpeleka hospitalini ambako alifanyiwa ukaguzi na madai yake yakathibitishwa.

Baadaye kisa hicho kiliripotiwa kwa afisa wa Idara ya Watoto katika kaunti ya Siaya, Beatrice Oguda.

Polisi walipashwa habari siku hiyo na mshukiwa akakamatwa.

Baada ya kuhojiwa kwa kina, msichana huyo aliwafichulia maafisa wa usalama kwamba babake pia aliwalawiti ndugu zake wa kiume.

“Maelezo ya kuhofisha kuhusu maovu ambayo watoto hutendewa na baba zao yametulazimu kuchukua hatua zinazohitajika,” akaeleza Bi Oguda.

Kesi hiyo iliwasilishwa rasmi mahakamani Siaya mnamo Juni 16, 2022.

Mshukiwa alishtakiwa kwa makosa manne mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Siaya.

Kosa la kwanza lilikuwa kunajisi binti yake huku makosa ya pili, tatu na nne yakihusu kuwalawiti wanawe wa kiume mara kadhaa.

Wakati alipowatendea watoto hao unyama, mshukiwa ndiye alikuwa akiishi nao na kuwalea baada ya mkewe kufariki mnamo 2020.

Katika uamuzi wake, Hakima Lester Simiyu alisema kuwa ushahidi tosha uliwasilishwa mbele yake kuthibitisha kuwa mshukiwa akimlazimisha bintiye kushiriki ngono ya mdomo kabla ya kumbaka.

Alirudia kitendo hicho kwa wanawe watatu wa kiume kabla ya kuwalawiti.

Hapo ndipo hakimu Simiyu akaamua hivi:“Baada ya masuala yote kuchunguzwa na mahakama hii imebainika kuwa mshukiwa amepatikana na hatia kwa makosa yote manne ya ubakaji na maovu mengine. Kwa hivyo nimemhukumu kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kwanza na miaka 10 kwa kila moja ya makosa mengine manne.”

Hii si mara ya kwanza kwa mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 51 kupatikana na hatia ya kuvunja sheria.

Kabla ya mkewe kufariki dunia, alizuiliwa katika rumande ya Gereza la Kisumu kwa kumlawiti mmoja wa watoto wake wa kiume.

Haijulikani ni jinsi gani aliachiliwa huru na akajiunga tena na familia yake.

Akijitetea, mshukiwa akana mashtaka yote dhidi yake na kuwakashifu majirani zake kwa kumwekelea makosa kutokana na wivu kwamba alipata mavuna mazuri.

“Majirani wameniwekelea mashtaka haya. Wananionea wivu kwa sababu nilipata mavuno mazuri mnamo 2020 kutokana kwa shamba langu la ekari nne. Nilivuna magunia 22 ilhali wengi walipata mavuno duni,” akaeleza.

Kulingana na ripoti iliyotolewa kabla ya uamuzi wa Hakimu kutolewa, Afisa wa Idara ya Uchunguzi katika Kaunti ya Siaya Lilian Odongo na kuwasilishwa mbele ya Bi Simiyu, mshukiwa amewahi kuhudumu gerezani kwa miaka miwili kwa kumshambulia kakake.