Babu Owino akaangwa kujilinganisha na Chamisa, Malema na Bobi Wine
Na PETER MBURU
WAKENYA mitandaoni wamemkemea mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, kwa kujaribu kujilinganisha na viongozi wanaoibuka barani Afrika, na kuvutia mamilioni kwa upekee wa uongozi wao.
Hii ni baada ya mbunge huyo kapitia akaunti yake ya Twitter Jumatano kudai kuwa alikuwa katika mazungumzo na viongozi wa kiafrika, yanayonuia kuliboresha bara.
Katika ujumbe wake, Bw Owino aliwarejelea kiongozi wa upinzani Afrika Kusini Julius Malema, wa Zimbabwe Nelson Chamisa na mbunge maarufu kutoka Uganda Bobi Wine kuwa wanazungumza kwa sauti moja.
“Ninafanya mazungumzio na Nelson Chamisa wa Zimbabwe, Julius Malema wa Afrika Kusini na Bobi Wine. Tunataka tuwe na sauti moja Afrika,” akasema mbunge huyo.
Lakini watumizi wa mtandao huo walimcheka kwa dharau Bw Owino kwa kujilinganisha na viongozi waliofahamika kote barani, ilhali yeye hajulikani popote. Wengine walimkashifu kwa kuungana na serikali alipotishiwa kidogo tu, haswa wakati imewakera Wakenya wengi.
“Pole, kwa bahati mbaya unafanya mazungumzo na wanaume ambao wamewacha alama kwa misimamo yao dhabiti dhidi ya wadhulumu, wezi na madikteta. Msimamo wako ni vituko, kuwa kibaraka, ubinafsi na ujeuri. Huna mwelekeo,” Alex Rango akamjibu.
Linah @Linah_NN alimwambia “Sauti gani? Uliogopa na kujiunga na wanaotudhulumu ili kuokoa kiti chako cha ubunge. Huwezi ukalinganishwa nao.”
Wengine walimtaka kujua viongozi hao watatu wana misimamo ya kuwatetea raia katika mataifa ya kwao, kinyume naye.
Ochivara Olungah alisema “amka kutoka ndoto hiyo kwa kuwa viongozi hao wanapendwa na watu kwa kuwa huwa wanawatetea, huwa wanazungumza kilicho katika akili zao na hawashirikiani na tawala ili kupata umaarufu, zaidi hawana tamaa ya uongozi.”
“Julius Malema si wa kiwango chako cha ubaraka ambacho kila kitu ni sawa kwako hata kama kinaumiza watu, bora tu ‘Baba’ amesema. Hata Bobi Wine ana msimamo dhabiti, anaposema Museveni ni mbaya, anamaanisha,” akasema Patrick Nyakoi.