BBI: Elimu ya uraia kufundishwa katika shule zote kote nchini
Na MARY WANGARI
SHULE zote nchini Kenya huenda zikaanza kufundisha somo la Elimu kuhusu uraia katika viwango vyote vya elimu kuanzia shule za chekechea hadi chuo kikuu endapo mswada wa ripoti ya Buiding Bridges Initiative (BBI) utaidhinishwa.
Kulingana na ripoti hiyo ya BBI iliyozinduliwa jana na Rais Uhuru Kenyatta katika Bomas of Kenya, Nairobi, shule za Kenya zitahitajika kujumuisha wanafunzi wote katika shughuli na majukumu yanayonufaisha shule na jamii yote kwa jumla.
Hatua hiyo itawezesha kukuza utamaduni wa kuwajibika na kutekeleza majukumu huku ripoti hiyo ikieleza kuwa pana tatizo kitaifa kuhusu utekelezaji na kukubali majukumu miongoni mwa watu binafsi.
Aidha, ripoti hiyo ilifafanua kuwa ili kukuza utamaduni wa uwajibikaji kwa kila Mkenya, ni sharti wananchi wahamasishwe kuanzia utotoni mwao kupitia mafunzo na elimu kuhusu kanuni za kijamii na kitaifa.
Shule vilevile zitahitajika kuruhusu na kuwezesha kujitolea kuwahudumia walio na mahitaji katika jamii au taasisi zilizo karibu na shule.
Ripoti hiyo pia ilipendekeza kuwa ni sharti raia wageuze mtazamo wao kutoka “nini taifa linaweza kutufanyia (haki) na kutilia maanani kile ambacho kila mmoja sharti afanyie taifa (majukumu yetu) ili kukomesha maovu kama vile ufisadi na udanganyifu.
Kulingana na ripoti hiyo kila Mkenya atakuwa na majukumu yafuatayo: Kutambua ukuu wa Mwenyezi Mungu wa maumbile yote, kuwaheshimu watu waliopigana vita kunyakua uhuru na haki ya taifa letu, kusherehekea na kuvumiliana kuhusu tofauti zetu kikabila, kitamaduni na kidini na kwa kufanya hivyo kuishi kwa amani kama taifa.
Majukumu mengine ni pamoja na kuheshimu na kudumisha mazingira yetu kama urithi tuliyopokezwa na tutakaokabidhi vizazi vijavyo, kuunga mkono kujitolea kustawisha na kulinda maslahi yetu binafsi na kila mtu kwa jumla.
Kutambua maazimio ya Wakenya wenzetu wote kuhusu serikali yenye utu, usawa, uhuru, demokrasia, haki ya kijamii, haki za kibinadamu na sheria, pamoja na kutekeleza haki zetu kama wananchi na haki za kuamua aina ya serikali nchini Kenya ni miongoni mwa majukumu yanayotarajiwa kutoka kwa raia.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa Wakenya wana haki zao kutoka kwa Mungu ambazo kwa sasa ni sharti ziambatane na Kanuni ya Kenya kuhusu Wajibu wa Raia inayotokana na Wimbo wa Taifa na Maadili ya Kitaifa, Kauli ya Raia kwa Taifa na Katiba ya Kenya kwa shule, sehemu za kazi, hafla rasmi na hafla za umma nchini.
Viongozi pia watahitajika kuwajibika ambapo kulingana na jopokazi hilo, mojawapo wa mahitaji ya kuwa waziri au katibu wa kudumu katika serikali ya kitaifa na pia katika kaunti, ni kuwa tayari kutumia huduma ambazo unaunda na kusimamia kwa niaba ya Wakenya wote.
“Ikiwa ni nzuri kutumiwa na Wakenya, inapaswa kuwa nzuri kutumiwa nawe,” inasema ripoti hiyo.
Kanuni ya Uwaziri itajumuisha mawaziri kutumia huduma kwa mahitaji yao binafsi au ya familia zao.
Kwa mfano, watoto wa Waziri wa Elimu wanapaswa kutumia shule za umma, Waziri wa Afya anapaswa kutumia huduma ya afya ya humu nchini na kadhalika.
Kulingana na ripoti hiyo, mawaziri wote wanafaa kutumia vituo na huduma za umma, hali ambayo vilevile inafaa kusawiriwa katika kaunti na mawaziri wa kaunti.