BBI: Masharti magumu kuhusu mchujo wa vyama
Na JUMA NAMLOLA
MAENEO Bunge yote 290 yataendelea kuwepo iwapo mapendekezo ya ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) yatakubaliwa na Wakenya.
Vile vile, nyadhifa maalum kama za walemavu zitahifadhiwa, kama njia ya kuleta usawa katika uongozi.
Hata hivyo, kwenye ripoti hiyo kuna mapendekezo ambayo huenda yakaondoa nafasi ya Mbunge Mwakilishi wa Kike.
Jopo hilo linasema kuwa tatizo ya uwakilishi wa jinsia litatatuliwa tu kwa kuvilazimisha vyama vya kisiasa kuzingatia usawa katika orodha zake za watu watakaowania nyadhifa mbalimbali.
“Vyama vitalazimishwa kupitia Sheria ya Vyama vya Kisiasa kufuata Katiba na kuwa na wanaume na wanawake kwa thuluthi mbili. Hili litafanya usawa huo upatikane, badala ya kuwa na uwakilishi wa kijinsia unaofanya ionekane kama mapendeleo,” inasema ripoti hiyo.
Haya ni kinyume na Mswada wa Punguza Mizigo, ambao ulikuwa umependekeza kuvunjwa kwa maeneobunge na kutumia kaunti 47 kama maeneo ya uwakilishi bungeni.
Aidha, Punguza Mizigo ilikuwa imetaka kila kaunti iwe na mbunge mwanaume na mwanamke, mbali na seneta.
Lakini huenda mambo yakawa magumu kwa wanasiasa wenye mazoea ya kuwahonga wasimamizi wa vyama na kupewa vyeti vya kuwania uchaguzi.
Ripoti ya BBI inataka mchujo wa kwanza ufanywe na wananchi katika maeneo wanakopanga kuwania.
Watu wanaotaka kuwania wadhifa wowote kupitia chama fulani, watajiwasilisha kwa wananchi wa eneo husika na kuchujwa, ili watakaosalia wamenyane kutafuta tikiti.
Hii ina maana kuwa, iwapo watu kumi watajitokeza, wananchi watawaondoa baadhi yao hata kabla hawajawasilisha vyeti vyao.
Inapendekezwa kuwa vyama vya kisiasa viwe na nguvu zaidi katika matawi ya kaunti, ambako wananchi watawasiliana na viongozi wao kupitia mijadala, sio tu wakati wa kampeni bali katika kipindi chote cha miaka mitano ya uongozi.
Kinachojitokeza zaidi kwenye mapendekezo hayo ni uwazi na kushirikishwa kwa wananchi.
Kupitia sheria hizi, vurugu za kila wakati wa mchujo wa vyama zitasahauliwa kwa kuwa ni wananchi watakaokuwa wamiliki halisi wa vyama vya kisiasa.