BBI: Matiang'i aonya polisi dhidi ya kutumiwa na wanasiasa
Na CHARLES WASONGA
WAZIRI wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i amewaonya maafisa wakuu wa usalama nchini dhidi ya kutumiwa vibaya na wanasiasa wakati huu wa mjadala kuhusu mageuzi ya katiba kupitia mapendekezo ya ripoit ya mpango wa maridhiano (BBI).
Aliongea Ijumaa alipofunga rasmi warsha ya siku mbili ya makamishna wa kanda na wale wa kaunti, Dkt Matiang’i pia waliwataka maafisa hao kuimarisha usalama kuhakikisha kuwa mdahalo wa BBI unaendeshwa katika mazingira ya amani.
“Mhakikishe kuwa sheria imefutwa bila mapendeleo. Lakini msikubali kutumiwa na wanasiasa vibaya wakati huu ambapo mjadala wa BBI umeshika kasi katika sehemu kadhaa nchini,” akasema.
“Kule nyanjani tutawasaidia viongozi wa kisiasa wakijadili masuala hayo na kuwashirikisha wananchi katika mjadala huo. Sio wajibu wetu kushiriki mijadala hiyo kuhusu BBI; hii ni kazi ya wanasiasa,” Dkt Matiang’i akakariri.
Hata hivyo, Waziri huyo alibainisha kuwa sekta ya usalama anayoiongoza inaunga mkono msimamo wa Rais Uhuru Kenyatta kuhusu ripoti ya BBI iliyozinduliwa mnamo Jumatatu wiki hii katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.
Maafisa wa usalama walilaumiwa mwezi huu pale walipofutilia mbali mikutano ya ambayo iliratibiwa kuongozwa na Naibu Rais William Ruto katika kaunti za Kisii na Nyamira, huku wakiruhusu mikutano wa wakereketwa kwa BBI kama vile kiongozi wa ODM Raila Odinga
Uzinduzi wa ripoti ya BBI ambao uliwaleta pamoja viongozi wa chama tawala cha Jubilee na vyama vya upinzani ulishuhudia kauli kinzani kuhusu ripoti hiyo; kati ya wanaoipinga na wale wanaoiunga mkono.
Dkt Ruto alikosoa mapendekezo kwenye ripoti hiyo haswa kuhusu kubuniwa kwa nyadhifa zaidi katika kitengo cha uongozi, na mabadiliko katika Idara ya Mahakama na Huduma ya Kitaifa ya Polisi.