BBI: Wafuasi wa Ruto wasema mkutano wa Naivasha haufai
Na CHARLES WASONGA
MASENETA wandani wa Naibu Rais William Ruto sasa wamepuuzilia mbali mkutano utakaofanyika Naivasha Jumapili, Novemba 1, 2020, kujadili kujadili muafaka kuhusu masuala tata katika ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI).
Wanasema mkutano huo wa maseneta na wabunge wa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga sio halali na ni “njama ya kufuja fedha za umma.”
“Sisi kama wabunge na maseneta wafuasi wa Dkt Ruto hatujaalikwa katika mkutano huo. Huo ni mkutano wenzetu wanaounga mkono BBI sio sisi ambao tumeeelezea kutoridhishwa na baadhi ya sehemu za ripoti hii,” Seneta wa Nandi Samson Cherargei akaambia Taifa Leo Ijumaa.
Kauli sawa na hiyo ilitolewa na Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa ambaye alipinga matumizi ya fedha za umma katika mkutano ambao alisema unalenga kuendeleza ajenda za wanasiasa wa mrengo wa Kieleweke.
“Waandalizi wa mkutano huo wa Naivasha wamevunja sheria kuwa kujadili ripoti ya BBI kabla ya kuwasilishwa rasmi bungeni. Hicho ni kikao kisichohalali na ambacho kinatumiwa kufyonza fedha za umma na kuendeleza ajenda ya kuwagawanya Wakenya kuhusu suala hili muhimu. Hii ndio maana sisi kama wafuasi wa Naibu Rais tumetengwa na hatukualikwa,” akaeleza.
Kwa upande wake seneta wa zamani wa Kakamega Bonni Khalwale alisema hakuna sheria inayoelezea namna mchakato wa BBI unapasa kuendesha kwa sababu ripoti hiyo haijawasilishwa rasmi bungeni.
“Kwa kutokuwepo kwa sheria kama hiyo mkutano wa Naivasha ni haramu. Kile wanapasa kufanya ni kupelekea ripoti hiyo bunge ili ijadiliwe huko wala sio mikahawani,” akasema.
Dkt Khalwale anashikilia kuwa ikiwa maswali ambayo Dkt Ruto aliuliza katika ukumbi wa Bomas, Jumatatu, mchakato mzima wa BBI utagonga mwamba.
Kiranja wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata jana alithibitisha kuwa wale walioalikwa mkutano huo wa Naivasha ni “wandani wa Rais Uhuru Kenyatta pekee.”
“Huu ni mkutano wa ‘Team Uhuru Kenyatta na Raila Odinga pekee’. Wale wengine ambao tuliwaona wakimwoshesha kiongozi wa taifa madharau katika Bomas juzi hawajaitwa,” akasema Bw Kang’ta ambaye ni Seneta wa Murang’a.
Duru zasema kuwa lengo la wafuasi wa Rais Kenyatta na Odinga ni kuzima uwezekano wa mageuzi zaidi kufanyiwa ripoti ya BBI inavyopendekezwa na wandani wa Dkt Ruto, baadhi ya wanasheria na viongozi wa makundi ya kutetea haki za kiraia.
“Nimeshiriki shughuli kama hii hapo awali na nimegundua kuwa sio jambo la busara kufungua stakabadhi kama hii kwa marekebisho zaidi. Ukifunge tena stakabadhi hiyo kwa marekebisho zaidi utarejea tena mahala ulikotoka, “ Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni alinukuliwa akisema.
Mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katika (CIOC) aliongeza kuwa muafaka unaotafutwa ni ule wa utaratibu wa utekelezaji ripoti hiyo ya BBI “wala sio kuhusu masuala mengine.”
“Niko katika kundi la wale wanataka tuitekeleze ilivyo kisha kuiimarishe baadaye. Wale wenye mawazo tofauti wanaweza kuyaleta ili yajumuishwe katika hatua ya kuimarisha ripoti hii wala sio kuifanyia marekebisho tena,” akaeleza Bw Kioni.
Kiongozi wa wachache John Mbadi aliseama ajenda ya mkutano huo wa Naivasha ambao utahudhuriwa na zaidi ya wabunge na maseneta 250 ni kuiwasilisha rasmi ripoti ya BBI bungeni.
“Kamati maalum ya BBI ilitekeleza wajibu wao na kumaliza kwa kuwasilisha ripoti kwa Rais Kenyatta na Bw Odinga. Sasa tutaelezewa yaliyomo kwenye ripoti hiyo ili tuipokee rasmi kupanga namna mapendekezo yaliyomo yatatekelezwa,” akasema Mbunge huyo wa Suba Kusini.
Wale ambao wanaunga mkono BBI wametambua uteuzi wa makamishna wapya wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) kuvunjwa kwa Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC) na wajibu wa Seneti katika kupitishwa kwa mswada wa ugavi wa fedha katika ya Serikali Kuu na zile za kaunti kama masuala muhimu ya kusaka muafaka kwayo.