Habari MsetoSiasa

BBI: Wandani wa Ruto wala njama ‘kumtega’ Uhuru

March 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ONYANGO K’ONYANGO

WAANDANI wa Naibu Rais William Ruto, wamepanga njama kutumia mkutano wa kuhamasisha Mpango wa Maridhiano (BBI) katika Kaunti ya Nakuru, kumshinikiza Rais Uhuru Kenyatta kutangaza wazi msimamo wake kuhusu uchaguzi wa 2022 ikiwa atahudhuria.

‘Taifa Leo’ imebaini kwamba viongozi hao wamekuwa wakimshinikiza Rais ahudhurie mkutano huo wa Nakuru ili ‘wamnase’ kwani amekosa kuitisha mkutano wa Chama cha Jubilee (JP) akiwa mwenyekiti wa chama.

Viongozi wanadai kuwa tangu handisheki kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM, Bw Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018, chama hicho kimeendelea kukumbwa na migawanyiko bila yeye kutoa kauli yoyote.

Wakiongozwa na wabunge Daniel Rono (Keiyo Kusini) na Caleb Kositany (Soy), viongozi walisema kuwa uwepo wa Rais Kenyatta utawapa nafasi kumuuliza msimamo wake kuhusu mpango wa urithi.

Walisema kuwa hawajaridhika vile mikutano ya awali kuhusu mpango huo imekuwa ikiendeshwa, kwani inaonekana kudhibitiwa na chama cha ODM.

“Mkutano wa Afraha utakuwa muhimu sana kwetu kama viongozi kutoka Bonde la Ufa, kwani tutautumia kumuuliza Rais ikiwa handisheki kati yake na Dkt Ruto mnamo 2012 ipo ama haipo.

“Vile vile, tutamtaka kueleza wazi kuhusu utaratibu ambao unatumika kuandaa mikutano ya BBI, kwani ilivyo sasa, mikutano hiyo inaonekana kuwa zoezi la ODM,” akasema Bw Rono, ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Ruto.

Kwa upande wake, Bw Kositany alisema kuwa ikiwa Rais Kenyatta hatokuwepo, basi Dkt Ruto ndiye anayepaswa kupokezwa mapendekezo eneo hilo lingetaka yajumuishwe kwenye ripoti hiyo. Alisema hawatayakabidhi mapendekezo hayo “kwa mgeni.”

“Huu ulikuwa mpango mzuri. Hata hivyo, mtu anayeupigia debe anafanya vibaya, kwani watu wengi hawaukumbatii. Kutokana na hayo, Rais Kenyatta anapaswa kutwaa udhibiti wa mikutano hii kwa haraka. Vile vile, anaweza hata kuisimamisha kwani imegeuka kuwa ya ODM,” akasema Bw Kositany.

Viongozi hao wamekuwa wakimshinikiza Rais Kenyatta kutangaza msimamo wake; kuhusu ikiwa atamuunga mkono Dkt Ruto mnamo 2022 au la.

Wameonya kwamba ikiwa mpango huo hautaendeshwa vizuri, basi utasababisha mkwamo wa kisiasa katika chama hicho.

“Ni wakati Rais Uhuru Kenyatta atangaze rasmi msimamo wake kuhusu yule atakayemrithi. Hili ni kwa kuwa baadhi yetu tunashikilia ahadi aliyotoa mnamo 2013, kwamba baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka kumi, atamuunga mkono Dkt Ruto kuiongoza nchi kwa miaka kumi. Binafsi, sioni lolote ambalo limebadilika,” akasema mbunge wa Endebess, Bw Robert Pukose.

Hata hivyo, mbunge wa Belgut, Bw Nelson Koech, alijitenga na wenzake kwamba Rais Kenyatta anapaswa kuhudhuria mkutano huo.

Alisema kuwa ikiwa pana haja wa Rais Kenyatta kuwaambia lolote, basi chama kinapaswa kuandaa mkutano wa viongozi.

Alieleza tashwishi yake kuhusu sababu ambapo maandalizi ya mkutano huo yanaendeshwa kisiri na kundi ambalo linaongozwa na magavana Alex Tolgos (Elgeyo-Marakwet) na Lee Kinyanjui (Nakuru).