Bei ya unga kushuka mahindi ya Mexico yakifika
Na PAULINE KAIRU
BEI ya unga wa mahindi inatarajiwa kushuka baada ya chama cha kampuni za kusaga unga kusema kuwa mahindi yaliyoagizwa kutoka Mexico yatafika nchini katika muda wa wiki mbili zijazo. Haya yanajiri baada ya serikali na kampuni hizo kuafikiana kuhusu masharti ya uagizaji.
“Tunatarajia shehena ya kwanza ya mahindi kuwasili nchini wakati wowote kuanzia kati mwa Juni. Yanatarajiwa kufikia kampuni zetu mapema Julai baada ya utaratibu wa kukaguliwa na kusafirishwa maeneo tofuati nchini,” Afisa Mkuu Mtendaji wa chama cha wasagaji unga Paloma Fernandes, aliambia wanahabari.
Serikali imeruhusu uagizaji wa magunia milioni mbili ya mahindi meupe kwa matumizi ya binadamu, na magunia mengine milioni mbili ya mahindi ya manjano ya kutengeneza chakula cha mifugo.
Mwezi Jana, kampuni za kusaga unga zilitahadharisha Wakenya kutarajia bei ya unga wa mahindi kupanda kwa Sh30 kwa pakiti ya kilo mbili kufuatia uhaba wa mahindi nchini baada ya Bodi ya Nafaka na Mazao (NCPB) kutangaza haikuwa na mahindi ya kuuzia kampuni hizo.
Awali, kampuni hizo zilikuwa zimezozana na serikali kwa muda wa mwezi mmoja kuhusu muda wa kuagiza mahindi baada ya serikali kuzipatia makataa ya Mei 30 ziwe zimeleta mahindi yote nchini. Kampuni hizo zilipinga agizo hilo zikisema ilikuwa vigumu kulitimiza.
Hatimaye, baada ya majadiliano, serikali ilikubali kuongeza muda hadi Julai 31. “Kwa sababu ya hatua hii, tunatarajia bei kushuka mahindi hayo yatakapowasili nchini,” akasema Bi Fernandes.