Benki ya Dunia yapiga jeki mpango wa Kazi Mtaani kwa Sh16.2 bilioni
Na BENSON MATHEKA
BENKI ya Dunia imepiga jeki mpango wa Kazi Mtaani nchini Kenya kwa kupatia serikali mkopo wa Sh16.2 bilioni kuimarisha huduma katika mitaa ya mabanda.
Taarifa kutoka benki hiyo Jumatatu ilisema kwamba pesa hizo zitasaidia kuimarisha usalama wa wamiliki wa nyumba katika mitaa ya mabanda nchini Kenya kwa kuwapa hatimiliki, kuimarisha barabara, mitaro ya majitaka, maji usafi, taa za barabarani na vyoo pamoja na kusaidia wakazi kukabiliana na hatari zinazowakabili likiwemo janga la corona.
“Benki ya Dunia imejitolea kuendelea kuunga juhudi za serikali za mpango unaoendelea wa Kazi Mitaani katika awamu zijazo hadi ufaidi vijana 200,000 katika kaunti zote 47,” alisema Sheila Kamunyori ambaye ni mtaalamu mkuu kuhusu miji wa benki hiyo.
Alisema kwa sasa, kazi ya kuimarisha barabara itatoa ajira kwa wakazi wa mitaa ya mabanda walioathiriwa na janga la corona.
Benki hiyo imesema pesa hizo zitafaidi wakazi 1.7 milioni wa mitaa ya mabanda iliyochaguliwa katika miji ya Kenya.
Ilifafanua kuwa zinatolewa kama ufadhili wa awamu ya pili ya mpango wa kuimarisha mitaa ya mabanda nchini Kenya (KISIP2).
“Mpango huu utakinga wakazi wa mitaa ya mabanda katika miji nchini Kenya ambao hutegemea mapato ya kila siku kujikimu dhidi ya athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la corona,”alisema meneja wa mipango wa benki ya dunia ambaye ni mkurugenzi wa benki hiyo nchini Kenya Camille Lampart Nuamah.
Serikali ya Kenya ilianzisha mpango wa Kazi Mtaani ili kuwakinga vijana katika mitaa ya mabanda dhidi ya athari za kiuchumi kufuatia janga la corona. Rais Uhuru Kenyatta alisema serikali imetenga Sh10 bilioni kufanikisha mradi huo hadi Desemba mwaka huu.