• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Benki ya Equity yatoa vifaa vya thamani ya Sh8 milioni kwa hospitali ya Thika Level 5

Benki ya Equity yatoa vifaa vya thamani ya Sh8 milioni kwa hospitali ya Thika Level 5

Na LAWRENCE ONGARO

BENKI ya Equity imetoa vifaa muhimu vya kuwakinga watu wakiwemo wahudumu wa afya (PPE) katika hospitali kuu ya Thika Level 5.

Mkurugenzi katika benki hiyo Bw Polycap Igathe, alisema kutokana na jinsi mambo yalivyo kuhusu Covid-19, benki hiyo kwa hekima yake imejitolea kuona ya kwamba wahudumu wa afya wote wanapokea magwanda maalum ya wao kutumia wakati wakifanya kazi yao.

“Sisi kama benki tumeguswa na kazi ngumu inayotekelezwa na wahudumu wa afya na kwa hivyo tumejitolea kuona ya kwamba madaktari na wasaidizi wao wanapata magwanda maalum ya kazi,” alisema Bw Igathe.

Baadhi ya vifaa vilivyotolewa ni viatu, barakoa, miwani, na nguo maalum za kuvalia za thamani ya Sh8 milioni ambazo alisema zitanufaisha wahudumu hao pakubwa.

Alisema alitumwa kupeleka vifaa hivyo na wakurugenzi wakuu wa benki hiyo Dkt James Mwangi na Bw Muthure Macharia ambao wamejitolea kuona ya kwamba benki hiyo inatoa misaada ya vifaa hivyo kwa kaunti zote nchini kwa gharama ya Sh1.1 bilioni.

Alisema benki hiyo imejitolea kufanya kazi kwa karibu na hospitali kadha za humu nchini kwa kuona ya kwamba zinapata vifaa vyote vya hospitali kwa wahudumu wote.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano alipozuru hospitali ya Thika Level 5 akiwa na wakuu wengine wa benki ya Equity.

Alisema Kenya inastahili kujivunia kuwa na viwanda vinavyoweza kuunda magwanda vinavyotumika katika hospitali za humu nchini.

“Baadhi ya viwanda hivyo ni wateja wetu na kwa hivyo tutaendelea kuwa na ushirikiano mwema navyo. Tuko tayari kutoa usaidizi utakaonufaisha Wakenya kwa jumla,” alisema Bw Igathe.

Naibu gavana wa Kiambu, Bi Joyce Ngugi alipongeza hatua iliyochukuliwa na benki ya Equity kwa kusaidia wahudumu wa afya.

“Tunaelewa madaktari wanapitia masaibu mengi wakati wakifanya kazi nzuri ya kuokoa maisha ya wananchi lakini baada ya kupokea vifaa hivyo watapata afueni kwa sababu kazi yao itakuwa rahisi kutekeleza,” alisema Bi Ngugi.

Alitoa mwito kwa wananchi popote walipo wafuate sheria zote zilizowekwa na idara ya afya ili kuweza kukabiliana na janga hili la Covid-19.

“Tunastahili kujihadhari kwa kufuata sheria zilizowekwa kwa sababu homa hiyo imeangamiza watu wengi wakiwemo madaktari wetu kadha,” alisema Bi Ngugi.

Wito watolewa

Waziri wa afya katika kaunti ya Kiambu Dkt Joseph Murega alitoa mwito kwa wananchi wajichunge na kuvalia barakoa kila mara wanapotembea popote pale. Pia alisisistiza umuhimu wa kunawa mikono ili kuepukana na homa hiyo.

“Kila mmoja wetu ana jukumu la kujihadhari na ni lazima tukubali ya kwamba ugonjwa huu uko miongoni mwetu.

Alisema tayari Kaunti ya Kiambu imetenga vitanda 800 mahususi kwa wagonjwa wa Covid-19 huku vitanda 16 vikiwa vya wagonjwa mahututi.

Daktari mkuu wa Thika Level 5 Dkt Jesse Ngugi alisema madaktari wanapitia wakati mgumu kutibu wagonjwa wa Covid-19 kwa sababu ya ukosefu wa magwanda muhimu ya wao kutumia.

Alisema matibabu ya wagonja wa Covid-19 ni ya gharama ya juu ikilinganishwa na  magonjwa mengine.

“Hata hivyo tumepongeza juhudi za benki ya Equity kutujali kwa kutufaa na magwanda muhimu ambayo tumekuwa tukitamani kupata,” alisema Dkt Ngugi.

Alisema kwa wakati huu wametenga wagonjwa 20 ambao bado wanaendelea kukaguliwa kutokana na homa ya Covid-19.

You can share this post!

Mchakato wa kupata saini za BBI wang’oa nanga

Nilimwachia Rashford apige penalti dhidi ya Basaksehir...