Habari Mseto

Biashara ndogo ndogo zawekewa ushuru mpya

September 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

Kufanya biashara katika Kaunti ya Mombasa sasa kutagharimu wafanyabiashara wadogo zaidi baada ya serikali ya kaunti hiyo kuanzisha kodi mpya kupitia Mswada wa Fedha wa 2018/2019.

Serikali ya Gavana Hassan Joho imeongeza na kuanzisha ada hizo mpya huku wakazi wakitarajiwa kuhusishwa katika mjadala wa kutekeleza mabadiliko hayo kabla ya kupitishwa na bunge la kaunti.

Hapo kesho, mamia ya wakazi watamiminika katika ukumbi wa Tononoka ambapo wakuu wa kaunti watajumuika nao kuzungumzia mswada huo wa fedha kabla upitishwe.

“Wakazi watasikizwa na kama kuna mabadiliko yatafanyika, wanatakiwa kuja kutoa maoni yao,” akasema mkurugenzi wa mawasiliano wa kaunti Richard Chacha.

Vijana wanaofanya kazi ya kuosha magari walipata pigo kubwa kufuatia mswada huo baada ya serikali hiyo ya kaunti kuanzisha ada ya kuwatoza kulingana na idadi ya mashini wanazotumia na watatakiwa kulipa kati ya Sh4,500 hadi Sh12, 000.

Wale wenye mashini tano za kuoshea magari na zaidi watalipa Sh12,000, kati ya mbili na tatu nao kutozwa Sh6,000 na wanaomiliki mashini moja kuwagharimu Sh4,500.

Shule za mitaa maarufu Community Based Schools zenye idadi ya wanafunzi 200 students watatozwa Sh25,000, zile zenye wanafunzi 100 hadi 200 kulipa Sh18,000 na zile zenye wanafunzi 100 kulipa Sh12,000.

Hata hivyo, wawekezaji wa sekta ya elimu walipinga mswada huo wakisema itamlimbikizia mzigo Mkenya wa mapato ya chini.

“Kaunti ya Nairobi tunalipa Sh10,000 kwa shule za mitaa wala si kutokana na idadi ya wanafunzi. Jamani Gavana Joho tunusuru kwa ada hizi,” akasema Bw Juma Lubambo mwekezaji wa shule za mitaani.

Kulingana naye, kuna zaidi ya shule 196 huko Mombasa zenye idadi ya wanafunzi 20,000.

“Nasafirisha nyanya kutoka eneo la Loitoktok kuja kuuza kwa wateja wangu ambao wengi wako kati kati mwa jiji la Mombasa huwa naegesha gari langu na kuanza kupanga bidhaa zangu kwa mifuko kabla kwenda kuwapelekea wateja wangu. Hivyo mimi hukwepa kulipa ushuru,” akasema Bw John Kimathi.

Bw Kimathi hana budi ila kukwepa ushuru kutokana na hali ngumu ya maisha hususan sasa ambapo bei ya mafuta imeongezeka.

Lakini atakuwa miongoni mwa wale ambao watatakiwa kulipa kodi hiyo.