Habari Mseto

Biashara zajiandaa kufungua

June 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

NA MISHI GONGO

WAHUDUMU wa hoteli na mikahawa jijini Mombasa wameanza matayarisho ya kufungua biashara zao wakitarajia Rais Uhuru Kenyatta atafungua shughuli za kiuchumi hivi punde.

Mwishoni mwa mwezi Machi serikali ilitoa agizo kwa mikahawa kutoruhusu wateja kuketi na kula sehemu hizo na badala yake kubeba chakula ili kuzuia watu kukongamana kama njia ya kudhibiti ugonjwa wa COVID 19.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya hoteli na mikahawa ililazimika kufunga milango yake kufuatia idadi ndogo ya wateja.

Akizungumza na Taifa Leo mhudumu katika mkahawa wa New life eneo la Kongowea, Bi Silvester Kanini alisema anamatumaini kuwa kusitishwa kwa marufuku kutaboresha uchumi wa nchi pakubwa.

“Tumekuwa tukipambana na kupotea kwa wateja kufuatia marufuku zilizowekwa, hata hivyo tuna imani kuwa baada ya tangazo la raisi mambo yatakuwa sawa.

Mhudumu mwengine katika mikahawa ya Chicken Inn, Bw Amos Omondi alisema kufungwa kwa baadhi ya kampuni na agizo la kuketi nyumbani kulichangia pakubwa kudorora kwa biashara yao.

Mratibu wa usalama katika eneo la Pwani, Bw John Elungata wiki iliyopita aliwahimiza washikadau kujitayarisha kuendeleza biashara zao hivi karibuni.

Alitaja baadhi ya matayarisho hayo kuwa wamiliki wa biashara hizo walipaswa kuhakikisha kuwa sehemu za kula zina nafasi ya kutosha kuwezesha wanaokula wasisongamane.

Aidha alisema japo marufuku yatasitishwa bado watu watapaswa kuvaa barakoa katika maeneo ya umma na pia kuzingatia kutokaribiana.

“Kusitishwa kwa marufuku kutamaanisha wageni kutoka mataifa mengine kuingia nchini, hivyo tunawaomba washikadau katika sekta ya utalii kuweka mikakati itakayohakikisha usalama wa wateja wao,”akasema.