Bingwa wa utoaji damu kwa ajili ya kuwasaidia wanaoihitaji awasili nchini
Na MAGDALENE WANJA
BINGWA wa utoaji damu dunia nzima kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wanayoihitaji Arjun Prasad Mainali amewasili nchini Jumanne.
Mainali anatarajiwa kuzuru sehemu mbalimbali wakati wa ziara yake na kampeni kuhusu umuhimu wa utoaji damu.
Umaarufu wake ni kutokana na utoaji damu wake ambapo ametoa mara 171.
Mainali amekuwa akizuru maeneo mbalimbali duniani katika kampeni za kuwahimiza watu kuhusu umuhimu wa kutoa damu.
Kulingana viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kipimo kimoja cha damu kinaweza kuokoa watu watatu na hivyo ameweza kuokoa maisha ya watu 513.
Shirika la Huduma za Utoaji Damu Nchini na Viungo vya Upandikizaji, Kenya National Blood Transfusion, Tissue and Human Organ Transplant Service, limeandaa shughuli ya utoaji wa damu kuanzia Septemba 9 hadi 13 kama njia ya kumuenzi bingwa huyo.
Kulingana na Kenya National Blood Transfusion Service (KNBTS), Bw Mainali atapokelewa na mabingwa wawili wa utoaji damu wa hapa nchini ambao ni Bw Alpha Kennedy Sanya na Bi Aisha Dafalla.
Bi Dafalla ametoa damu mara 64 huku Bw Sanya akitoa mara tisa.