BOBI WINE: Shinikizo kwa Museveni aachilie huru msanii zazidi
Wandamanaji hao, wakiwemo wanaharakati wa Kenya, wanamuziki na wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka Kenya na Uganda walishutumu vikali hatua ya serikali ya Uganda na kutaja hatua ya kumshtaki na kumfikisha mahakamani kama ukiukaji wa haki za kibinadamu na kuvunja sheria za Umoja wa Kimataifa.
Walitumia vipaza sauti, mabango na nyimbo za msanii huyo za kisiasa na kutaja kwamba wanapigania uhuru wa nchi ya Uganda, ambayo wanadai imo gizani kwa uongozi wa kiimla.
“Hakuna uhuru Uganda, wakati wa dikteta Museveni kuondoka uongozini umewadia. Yeye na familia yake. Mateke anayorusha ni ya punda. Haya ni mateke ya mwisho,” akasema Joseph Subuga ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Aidha wanataka mataifa yaliyostawi na Umoja wa Kimataifa kuingilia kati na kuiwekea Uganda vikwazo.
“Tunataka Museveni atambue kuwa kamwe yeye hawezi kuishi bila vikwazo kutoka Umoja wa Kimataifa. Awe tayari kupokea vikwazo kutoka kwa mataifa yaliyostawi. Uganda sio nchi yake bali ya wananchi wengi. Lazima atii sheria,” akafoka mmoja wa waandamanaji, Janet Kisila.
Mwanamuziki huyo na wengine 30 walitiwa nguvuni na wengine wenzake 30 katika mji wa Arua wiki iliyopita kwa madai ya kumiliki silaha. Mashtaka mapya dhidi ya mwanamuziki huyo ni kujaribu kuua bila kukusudia.