Bodi ya NHIF ilitumia Sh38 milioni kwa mikutano – Mhasibu
Na SAMWEL OWINO
IMEBAINIKA kwamba Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) ilitumia Sh38 milioni za walipa ushuru kuandaa mikutano ya bodi, warsha na makongamano mwaka 2018.
Ripoti ya aliyekuwa mkaguzi wa hesabu za serikali Edward Ouko katika mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 2018 ilibainisha kwamba, NHIF ilitumia pesa hizo lakini ikakosa kuonyesha stakabadhi za kuthibitisha matumizi hayo.
Kulingana na stakabadhi zilizopelekwa mbele ya kamati ya uwekezaji katika Bunge la Kitaifa, kati ya fedha hizo, Sh13,115,573 zilitumika kuandaa warsha na makongamano.
Vilevile, hazina hiyo iliwalipa maafisa wawili Sh993,220 kama marurupu ya usafiri kwa kuhudhuria kongamano la ugatuzi mjini Kakamega na maonyesho ya kilimo jijini Mombasa.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba, Sh3, 923,119 zilitumika kugharimia mikutano ya wanachama wa bodi ya NHIF japo Bw Ouko alikosoa NHIF kwa kutotoa stakabadhi za malipo hayo.
“Ingawa usimamizi umefafanua kwamba pesa hizo zilitumika kugharimia mikutano ya bodi, hakukuwa na ushahidi kuthibitisha matumizi hayo,” ikasema ripoti ya Bw Ouko.
Pia ilisema Sh4,633,631 zililipwa kwa chuo cha Havard nchini Amerika kwa kutoa mafunzo kwa wanachama wawili wa bodi kuhusu masuala ya uongozi.
Stakabadhi
Hata hivyo, ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali ilionyesha kwa NHIF haikutoa stakabadhi zilizoonyesha kwamba mafunzo ya wawili hao yaliidhinishwa na wanachama wote wa bodi.
Maswali hata hivyo yaliibuliwa na afisi ya mkaguzi wa hesabu kwa nini wanachama hao wawili hawangepokea mafunzo hayo nchini ili kuokoa fedha za walipa ushuru.
Kwenye barua iliyoandikwa Juni 18, 2018, aliyekuwa kaimu katibu wa NHIF Ruth Makallah aliomba bodi iidhinishe fedha za kugharimia mafunzo kwa maafisa hao, zoezi ambalo lilifanyika tarehe tofauti mnamo Julai 2018.