• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 1:24 PM
Boinnet ateua makamanda wapya wa maeneo manane

Boinnet ateua makamanda wapya wa maeneo manane

Na BENSON MATHEKA

Inspekta Jenerali wa polisi, Joseph Boinnet, ameteua wakuu wapya wanane wa polisi katika juhudi za kuimarisha usalama nchini na kubadilisha huduma ya polisi.

Kwenye uteuzi huo, Bw Philip Ndolo atasimamia Nairobi, Judy Jebet Lamet atachukua wadhifa huo eneo la Kati na Edward Mwamburi atashirikisha shughuli za polisi eneo la Rift Valley.

Bw Boinnet alimteua Marcus Ochola kusimamia eneo la pwani, Eunice Kihiko (Mashariki) Paul Soi (Kaskazini Mashariki), Rashid Yakub (Magharibi) na Dkt Vincent Makokha (Nyanza).

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Bw Boinnet alisema kwamba maafisa waliokuwa wakihudumu maeneo hayo watapatiwa kazi zingine katika huduma ya polisi.

Baadhi ya maafisa hao ni Joseph Ole Tito aliyekuwa akisimamia Nairobi, Noah Mwaviwanda (pwani), Julius Kitili (Magharibi), Francis Munyambu (Kati) na Moses Ombati (Mashariki)

“Hakuna atakayepoteza kazi, tutawaita na kuwapatia majukumu mapya katika huduma ya polisi,” alisema Bw Boinnet. Aliwahakikishia kuwa hawatapoteza vyeo vyao wakipatiwa majukumu mapya. Bw Boinnet alisema walizingatia usawa wa jinsia, umri, tajiriba na usawa wa kimaeneo katika kuteua maafisa hao wapya. “Tulizingatia mambo mengi katika kufanya uteuzi huu. Tulichunguza rekodi za mtu, tajiriba, umri, eneo analotoka na jinsia,” alisema.

Bw Boinnet alitangaza kuwa mabadiliko makubwa yatafanyiwa makamanda wa polisi wa kaunti kama njia moja ya kutekeleza mageuzi katika huduma ya polisi ambayo Rais Kenyatta alitangaza Septemba mwaka jana.

“Tutatoa tangazo kubwa kuhusu makamanda wa kaunti hivi karibuni,” alisema Bw Boinett.

Alisema makamanda hao wapya watasimamia operesheni zote za polisi na kushirikisha makamanda wa kaunti zitakazokuwa chini ya maeneo yao ili kuimairisha usalama.

Katika hatua za kuweka vikosi vya polisi wa kawaida na wale wa utawala chini ya usimamizi mmoja, Bw Boinnet alitangaza kuwa makamanda wote wa maeneo ya vikosi hivyo wataondolewa ili kutoa nafasi ya wapya alioteua.

“Ninataka kuhakikishia Wakenya kwamba, mageuzi ya polisi yanaendelea. Tumeanza kutekeleza maagizo tuliyopatiwa na Rais Uhuru Kenyatta mwaka jana na kwa wakati huu tunapozungumza, polisi walipokea marupurupu ya nyumba kuanzia mwezi uliopita,” alisema.

Kulingana na Bw Boinnet, marupurupu ya nyumba ya maafisa wa polisi yaliidhinishwa na Tume ya Mishahara (SRC).

Bw Boinnet alitangaza kuwa kuanzia Januari 17, rekodi katika vituo vya polisi zitakuwa za kidijitali. Waziri wa usalama wa ndani atazindua huduma hizo Kaunti ya Kilifi Januari 17 mwaka huu. “Tunahamia mfumo wa kidijitali na tutalenga maeneo matatu ambayo ni usimamizi, vitabu vya matukio na usimamizi wa rekodi za uhalifu,” alisema Bw Boinett.

Alisisitiza kuwa maafisa wa polisi watapatiwa sare mpya ambazo zitangenezewa nchini na Shirika la Vijana wa Huduma kwa Taifa (NYS).

Jana, Bw Boinnet aliandamana na manaibu wake wawili, Edward Mbugua, Noor Gabow (AP), Mkurugenzi wa upelelezi wa jinai George Kinoti na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Huduma ya polisi George Onyango.

You can share this post!

Heroini: DPP ataka mshukiwa aozee jela miaka miaka 22

Viongozi wakataa utaratibu wa kugawa fedha za kaunti

adminleo