Breki kwa marufuku ya matangazo ya kamari
MAUREEN KAKAH na CECIL ODONGO
WATU maarufu wako huru kushiriki katika matangazo ya michezo ya pata potea.
Hii ni kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu kusimamisha kwa muda marufuku iliyowazuia watu maarufu kuhusishwa katika matangazo ya kamari.
Marufuku hiyo ilitolewa na Bodi ya Kudhibiti Kamari nchini (BCLB) kama njia mojawapo ya kuzuia Wakenya kupata uraibu wa kucheza michezo ya patapotea.
Jaji James Makau alisitisha marufuku hiyo baada ya msanii kwenda mahakamani akidai kuwa inahatarisha mapato yake.
“Marufuku hiyo iliyotolewa na bodi ya BCLB mnamo Aprili 30, 2019 imesitishwa hadi pale kesi hii itasikizwa na kuamuliwa,” akasema Jaji Makau.
Marufuku hiyo iliyoanza kutekelezwa Mei 30, ilipiga marufuku kutangazwa kwa kamari kwa kutumia mabango na kwenye mitandao ya kijamii. Pia ilikataza matangazo ya michezo ya kamari kati ya saa 12 asubuhi na saa 4 usiku
Kesi hiyo iliwasilishwa na Bw Kamau Wanjohi, maarufu MC Moreydoc.
Amemshtaki mwenyekiti wa bodi Bw Cyrus Maina na mkurugenzi mkuu Liti Wambua na Mkuu wa Sheria.
Kulingana na msanii huyo, marufuku hiyo ilitolewa bila bodi hiyo kushauriana na Wakenya. Utata kuhusu mtu anayefaa kuitwa ‘maarufu’ umetoa mwanya kwa watu kuendelea kushiriki katika matangazo ya michezo ya kamari.
Wakati wa kutangaza marufuku hiyo, Bw Wambua alisema kuwa mabango ya matangazo yalifaa kuwa na maandishi ya kuonya watu dhidi ya kujitosa katika kamari.
Marufuku hiyo ya BCLB, ilizuia watu maarufu kama vile mchezaji wa kandanda Macdonald Mariga, Joey Muthengi, Janet Wanja na Carol Radull kutoshiriki katika matangazo ya michezo ya kamari.
Kwengineko, waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i jana aliamuru ukaguzi wa kina ufanyiwe kampuni za kamari zinazotafuta leseni za kuhudumu huku ikibainika zinadaiwa Sh20bilioni na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru(KRA).
Dkt Matiang’i alisema masharti ya ulipaji ushuru ndiyo yatatumiwa kama msingi wa kutoa lesini kwa kampuni yoyote ya mchezo wa pata potea nchini.