Bunge lamtaka Mwende kuasi uraia wa Amerika
Na CHARLES WASONGA
BUNGE la Kitaifa Alhamisi jioni lilipitisha ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni iliyowapiga msasa watu saba walioteuliwa kuwa mabalozi wa Kenya katika mataifa ya ng’ambo lakini kwa sharti moja kuhusu Bi Mwende Mwinzi.
Ripoti hiyo iliidhinisha uteuzi wa Bw Mwinzi kuwa balozi wa Kenya nchini Korea Kusini lakini kwa sharti kwamba aasi uraia wake wa Amerika kabla ya kuchukua wadhifa huo.
Kuidhinishwa kwa uteuzi wa Bi Mwinzi kwa sharti hilo kulipingwa vikali na wabunge wanawake wakiongozwa na Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo.
“Hii sio haki. Mbona Bi Mwinzi anawekewa sharti hilo ilhali yeye ni Mkenya. Ama ni kwa sababu yeye ni mwanamke. Hitaji hilo liondolewa mara moja na jina lake liwasilishwa kwa rais pamoja na wenzake kwa uteuzi rasmi,” akasema Mbunge huyo wa ODM.
Kauli yake iliungwa mkono na wabunge wenzake wa kike, Bi Sicily Mbarire, (Mbunge Maalum), Esther Wahome (Kandara) na Florence Mutua (Mbunge Mwakilishi wa Busia).
Lakini kulingana na Sheria ya Uongozi na Maadili afiosa wa serikali ambaye atachukua uraia wa mataifa mawili atapoteza nafasi hiyo.
Kulingana na sheria hiyo, mtu ambaye ana uraia wa mataifa mawili ikiwa atachaguliwa au kuteuliwa kama afisa wa serikali hawezi kuchukua wadhifa huo hadi pale atakapoasi uraia wa taifa la pili kulinga na Sheria ya Kenya kuhusu Uraia na Uhamiaji.
Hii ndio maana wabunge sasa wanashikilia kuwa sharti Bi Mwinzi aasi uraia wake wa Amerika kabla ya kusafiri hadi Seoul kuwakilisha Kenya kama balozi.
Wengine ambao uteuzi wao uliidhinishwa na wabunge ni; naibu afisa mkuu mtendaji wa EACC anayeondoka Michael Mubea ambaye ataenda jijini Dublin nchini Ireland, Kariuki Mugwe (Abu Dhabi), Peter Angore, (Algiers, Algeria) Flora Karungu (Lusaka, Zambia), Diani Kiambuthi (Stockholm, Uswidi) na Njambi Kanyungu (UN-Habitat).
Sasa majina ya sita hao, isipokuwa Bi Mwinzi, yatawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta ili awateue rasmi.