CDF: Wabunge 14 wamulikwa kuhusu Sh1 bilioni
Na DAVID MWERE
KWA mara nyingine wabunge 14 wamejipata pabaya kuhusiana na matumizi mabaya ya zaidi ya Sh1 bilioni, fedha za hazina ya ustawi wa maeneobunge yao (NG-CDF) kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Ripoti hiyo ya matumizi fedha mwaka wa kifedha 2017/2018 ambayo wakati huu inachambuliwa na Kamati ya Bunge kuhusu Matumizi ya Fedha za Hazina Maalum, inawalaumu wabunge hao kwa kutosimamia fedha hizo vyema.
Wabunge ambao wanalaumiwa kwa kutozuia wizi wa pesa za NG-CDF katika maeneobunge yao ni pamoja na Oscar Sudi (Kapseret), Alloice Lentoimaga (Samburu Kaskazini), Emmanuel Wangwe (Navakholo), Mark Nyamita (Uriri), Benard Shinali (Ikolomani), Jeremiah Lomorukai (Loima) na Julius Melly (Tinderet).
Wengine ni; Aisha Jumwa (Malindi), Alpha Miruka (Bomachoge Chache) John Oyioka (Bonchari) na Vincet Kemosi (Mugirango Magharibi).
Kulingana na uchunguzi, ofisi ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, hakuna stakabadhi zilizowasilishwa kuthibitisha pesa zililipwa hali ambayo inaibua wasiwasi kwamba huenda pesa ziliibiwa. Katika maeneo mengine, fedha zilitengwa kwa miradi ambayo inachukua muda mrefu kukamilishwa, ilikwama ama haiko. Na katika baadhi ya maeneo bunge, fedha zilitengwa kwa miradi licha ya kutokuwepo kwa kamati za kusimamia miradi hiyo.
Kwa mfano, katika eneobunge la Kapseret linalowakilishwa na Bw Sudi, ripoti hiyo inasema kuwa jumla ya Sh69,626 hazijulikani zilivyotumiwa katika mwaka wa kifedha wa 2017/2018.
Aidha, miradi 40 haijakamilishwa licha ya kutengewa Sh56.426 milioni bila sababu maalum kutolewa kwa hali hiyo. Na licha ya Sh5 milioni kutumiwa kununua vipande vya ardhi kwa matumizi ya shule kadhaa katika eneobunge, hakuna hatimiliki zilitolewa kuthibitisha kuwa vipande hivyo vilinunuliwa.
Na katika eneobunge la Samburu Kaskazini, matumizi ya jumla ya Sh46.65 hayawezi kuthibitishwa.
Aidha, Sh14 milioni zilitumika kwa basari lakini hamna barua kutoka kwa waliofaidi kuthibitisha walipokea pesa hizo.
Katika eneobunge la Navakholo lake Bw Wangwe, Sh51, 355 zilitumika kwa miradi ambayo imechelewa kukamilishwa licha ya fedha za CDF kutochelewa kutumwa.