Habari Mseto

Changamoto katika kuafikia ajenda ya afya bora kwa wote

May 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

ILI kufanikisha ndoto ya Rais Uhuru Kenyatta ya kuafikia afya bora na kwa bei nafuu kwa Wakenya wote, lazima kutengwe Sh350 bilioni kuanzia sasa hadi mwaka wa 2021, hali ambayo katika ugumu wa kiuchumi, huenda lisiafikiwe.

Haya yamefichuliwa na menyekiti wa kamati ya afya bungeni, Sabina Chege ambaye amekiri kuwa “kuafikia ajenda hii haitakuwa kazi rahisi.”

Katika bajeti inayotarajiwa kuandaliwa ya 2019/20, Wizara ya Afya imetengewa Sh93 bilioni ambapo ufanisi wa ajenda hii ya afya umetengewa Sh35.8bn.

Hii ina maana kuwa ajenda hii inatarajiwa itengewe zaidi ya Sh305.2 bilioni katika bajeti za 2020/21 na 2021/22 na ambapo Rais Uhuru Kenyatta atakuwa akiondoka mamlakani baada ya kuongoza kwa awamu mbili Ikulu.

“Rais ako tu na utekelezaji wa bajeti za 2019/20 na 2020/21. Ina maana kuwa tuko na safari ya kuendelea kusaka ufanisi wa ajenda hii hata baada ya rais Kenyatta kuondoka ikulu,” akasema.

Alisema kuwa ugumu huo wa kuafikia ajenda hii utajidhihirisha katika majadiliano ya hospitali za hapa nchini kupunguza gharama za kimatibabu, uadilifu wa wahudumu wa kiafya wawe wa kuzingatia maisha ya Wakenya badala ya kugoma mara kwa mara na pia bima za kiafya zikilainishwa ili ziwafae Wakenya wote kwa usawa.

Alisema kuwa kuna pendekezo kuwa bima ya afya ya serikali (NHIF) itathiminiwe upya ili itenge walio na umaskini mkuu kutokana na ada na wawe wakigharamiwa matibabu, kuwe na usawa wa kulipia bili za kimatibabu katika hospitali za hapa nchini na ng’ambo na pia vijana wa kati ya miaka 18 na 35 wapunguziwe ada hadi Sh100 kwa mwezi.

Bi Chege alisema kuwa kwa sasa gharama ya kutibiwa katika chumba cha hali mahututi ni kati ya Sh40,000 na Sh180,000 kwa siku akisema kuwa gharama hiyo inamaanisha mauti kwa wengi kwa kuwa hawawezi wakaimudu.

“Ndio unapata visa hapa nchini vya utapeli wa wazi ambapo hospitali zinaweka mgonjwa mahututi katika mashine ya kumsaidia kupumua kwa miaka miwili, kisha anafariki akiwa na bili ya kati ya Sh20 milioni na Sh100 milioni na kisha inakatalia mwili eti kwanza bili hiyo sharti ilipwe,” akasema.

Alisema kuwa gharama ya kupachikwa figo mpya inagharimu mgonjwa wa Kenya kati ya Sh500,000 na Sh1.5 milioni akisema kuwa ni lazima kuwekezwe rasilimali kwa utaalamu na vifaa hapa nchini na kisha gharama ipunguzwe ili wengi wapate hakikisho la afya bora kwa wote.

Alisema kuwa ikiwa huduma za kiafya zitazidi kuwa mikononi mwa serikali za kaunti, kuna uwezekano mkuu kuwa ajenda hii itafeli.

“Kwa sasa hakuna mikakati ya kushinikiza kuwa ile pesa ya bajeti serikali kuu hutuma kwa manufaa ya hospitali za Kaunti lazima itumike kufadhili huduma za kiafya. Gavana akiwa mtundu atatumia pesa hizo kupiga siasa,” akasema.

Bi Chege alisema kuwa kwa sasa mlima ambao Kenya inahitaji kukwea ili ifanikiwe ni mkubwa kiasi kwamba ni matumaini na dua njema itanusuru hali.