Chokoraa 36 wataka waelezwe waliko wenzao 5
NA RICHARD MAOSI
CHOKORAA wanaozurura mjini Nakuru, sasa wanataka kuelezewa waliko wenzao watano kati ya 41 waliotupwa eneo la Torongo, Kaunti ya Baringo wiki mbili zilizopita.
Hili linajiri wiki moja tu baada ya mbunge wa zamani wa Naivasha John Mututho kuwaokoa vijana 36 kati ya 41 waliotelekezwa, huku wengine watano wasijulikane waliko.
Kulingana na msemaji wao Josephat Koech ,wamekuwa wakihangaishwa na polisi mara ya kwanza waliachwa katika eneo la Kabazi, kisha Naivasha na baadaye Baringo.
Koech alionyesha hofu akisema sio haki kuwatendea unyama , kwani baadhi ya watoto hao walikuwa wachanga na wengine walemavu.
Wiki iliyopita vijana hao walipata habari kuhusu mmoja wao aliyeaga dunia baada ya kuumwa na nyoka,lakini juhudi zao kumpata katika vyumba vya kuhifadhi maiti hazikuzaa matunda.
“Tumezunguka hospitali zote za Nakuru,tukiulizia habari za mwenzetu bila mafanikio yoyote,”alisema.
Joseph Kamau ni mmoja wa wale waliotupwa katika eneo la Torongo,lakini alifanikiwa kutafuta njia ya kumfikisha Nakuru siku ya Alhamisi kwa miguu.
“Nilitembea mwendo mrefu wa siku tano hadi nilipofika Nakuru na kupokelewa na wenzangu waliodhani nimeaga,”Kamau alieleza.
Koech alieleza kuwa vijana wengi walitoroka makwao kwa sababu ya changamoto za familia.
Aliahidi kuanzia sasa hawatakubali tena kutumika na viongozi ili kuendeleza ajenda zao za 2022.
Aidha anaomba Gavana Lee Kinyanjui atimize ahadi ya kutoa ajira kwa vijana kama alivyosema katika kampeni zake za 2017.
“Baadhi ya vijana tayari walikuwa wamejiandikisha kwenye ofisi ya Disii kusomea taaluma za kiufundi lakini walijing’atua pindi walipoombwa 5000 kila mmoja,”Ibrahimu Karanja aliongezea.