Habari Mseto

CHRISTINE NJERI: Napania kutinga upeo wa Jenniffer Lawrence

August 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

‘MGAAGAA na upwa hali wali mkavu,’ ni methali inayohimiza wanadamu kutovunjika moyo kwenye harakati za tamanio la kutimiza malengo fulani maishani mwao.

Ni methali inayozidi kuthibitishwa na wengi wanaoendelea kuchangamkia shughuli mbali mbali kwenye juhudi za kusaka riziki. Kati yao ni mwanadada Christine Njeri Wangiabi mwigizaji anayekuja anayepania kutinga upeo wa kimataifa miaka ijayo.

”Ingawa sijapata mashiko katika sanaa yangu ndani ya miaka mitano ijayo nalenga kuwa katika kiwango cha kushiriki filamu za Hollywood kama ilivyo kwa Mkenya, Lupita Nyong’o aliyejizolea umaarufu tele kupitia filamu yake kwa jina ’12 Years a slave.’

Kadhalika analenga kujiunga na Taasisi ya Yale School of Drama kupata elimu zaidi kuhusu masuala ya maigizo kwenye juhudi za kutimiza matumaini yake ndani ya kipindi hicho.

Mwigizaji huyu anasema alivutiwa na uigizaji akiwa mdogo baada ya kutazama msanii mahiri, Maite Peroni aliyeshiriki Triumph of Love Soap Opera.

”Sina shaka kutaja kwamba msanii huyo ndiye aliyenipa motisha zaidi katika uigizaji,’ anasema na kuongeza kwamba anaamini yupo katika mwelekeo mzuri. Dada huyu ambaye bado amepania kuhitimu kuwa wakili anasema anatamani sana kuzamia masuala ya uigizaji anakolenga kutinga hadhi ya msanii mahiri duniani, Jenniffer Lawrence mzawa wa Marekani.

SCRIPT

Binti huyu aliyezaliwa mwaka 1999 hufanya kazi na kundi la Zawadi productions ambalo huandaa shoo zake katika ukumbi wa Kenya National Theatre (KNT). Msanii huyu anajivunia kushiriki filamu nyingi tu ambazo huonyeshwa kwenye ukumbi huo chini ya kundi hilo tangia mwaka 2007. Kadhalika anajivunia kushiriki filamu moja kwa jina ‘Kina’ iliyopata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga ya Maisha Magic plus.

”Kando na uigizaji ninajivunia kuwa mwandishi wa script za filamu taalamu ninayolenga kuzamia bila kulegeza kamba,” alisema na kuongeza kwamba anafahamu hakuna kizuri hupatikana rahisi.

Anasema kupitia muungano wa kundi bora ambalo huzalisha filamu na kuzitupia katika mtandao wa kijamii wa You tube ameandika script za filamu mbili:’Cindy,’ na ‘Morals.’

PEARL THUSI

Mwigizaji huyu pia anajivunia kutwaa tuzo ya ‘Best Supporting Actress’ mwaka 2015 kwenye hafla iliyoandaliwa na muungano wa makanisa kwa jina Lavington United. Anasema bado ana kiu cha kunasa tuzo nyingine katika maigizo ya upeo wa juu kando na kanisa.

Kisura huyu anasema angependa sana kufanya kazi na kati ya waigizaji mahiri duniani akiwamo Pearl Thusi mzawa wa Afrika Kusini aliyejizolea umaarufu katika kipindi chake kiitwacho ‘Queen sono,’ pia Mercy Johnson ambaye huigiza katika filamu za Kinigeria ‘Nollywood.’ Kwa wasanii wa humu nchini angependa kufanya kazi na Brenda Wairimu bila kumsahau Kate Actress. Anashukuru Mungu kwa kumpa kipaji cha uigizaji, mamake mzazi Mary Njeri kwa kumuunga mkono katika taaluma yake bila kuweka katika kaburi la sahau wafuasi wake.

Kisura huyu anahitaka serikali ianzishe kumbi za maigizo katika Kaunti zote 47 ili kupunguza idadi ya waigizaji wanaofurika katika miji mikuu ikiwamo Nairobi na Mombasa kati ya mingine. Anadokeza kuwa Kenya ina waigizaji wengi tu hasa kule mashinani lakini kwa kukosa nafasi kuonyesha ujuzi wao talanta zao huyeyushwa na masuala mengine pengine yasiona na manufaa kwao.