Habari Mseto

Chuma ki motoni kwa maafisa wa serikali walevi

June 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANGI MUIRURI

KAMISHNA wa Kaunti ya Murang’a, Mohammed Barre ameagiza misako itekelezwe dhidi ya watumishi wa umma ambao watapatikana wakiwa walevi kupindukia katika mji huo.

Akiongea afisini mwake Jumanne jioni baada ya kuongoza kikao cha kupanga mikakati ya usalama wa eneo hilo alisema walimu, matabibu na pia maafisa wa idara mbalimbali za polisi ndio wameongoza katika ukosefu wa tabia katika ulevi.

Aliagiza wakabiliwe vilivyo katika miji ya eneo hilo hasa masaa ya kazi.

“Itakuaje raia warekebishe mienendo yao ya kulewa kupindukia ikiwa wanaofaa kuhakikisha maadili mema katika jamii na pia wadumishaji sheria ndio wakiwakilisha sura ya serikali ndio wameongoza katika utovu wa nidhamu ndani ya ulevi?” akanuna.

Alisema wengi wa watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na wanawake huwa wanalewa kupindukia na kuzua kila aina ya aibu katika baa za kaunti hiyo.

“Wengine huwa wanatoka Kaunti zingine kushiriki ulevi hapa na wakiporwa katika baa huishia kulala nje ya hospitali kuu ya Murang’a huku wakidai wana wagonjwa ndani ya wodi ili asubuhi ikiingia wasake mbinu za kufika makwao. Wasimamizi wa hospitali hii wanafaa kuwa wanaita polisi wakiona watu kama hao ambao maadili ya taaluma yamewaishia,” akasema.

Mkutano huo uliazimia kuwa misako itekelezwe dhidi ya magari ya uchukuzi ili kuzima ajali za barabara na pia wahudumu wa bodaboda wamulikwe ili kuzima ukora miongoni mwao wa kuwaibia wateja wao.

Aidha, waliazimia kuwa macho katika vijiji ili kuwatambua wakora ambao wanatafutwa na polisi kwa uhalifu mbalimbali hapa nchini, hasa maharamia ambao tayari wametolewa ilani ya kufurushwa na serikali kuu.