Corona: Hatua ya landilodi kuwaondolea wapangaji kodi yachangamsha wengi
Na MACHARIA MWANGI
MMILIKI mmoja wa nyumba mjini Ndunyu Njeru katika eneobunge la Kinangop, Kaunti ya Nyandarua, amewaondolea kodi ya nyumba wapangaji wake kwa miezi miwili katika juhudi za kuwapunguzia makali ya kiuchumi yanayotokana na virusi vya corona.
Mmiliki huyo, Michael Munene, ambaye ni mfanyabiashara eneo la Kinangop, aliwaambia wapangaji hao watumie pesa ambazo wangemlipa kwa miezi hiyo miwili kununua chakula kwa familia zao wakati huu mgumu.
Kutokana na kitendo hicho cha hisani, mfanyabiashara huyo anayemiliki nyumbani za biashara na makazi, atapoteza mapato takriban Sh100,000 kila mwezi.
“Aliwaita wapangaji wote Jumamosi ndipo akatoa tangazo hilo ambalo limetupa afueni kubwa zaidi,” akasema Peter Muya, mmoja wa wapangaji wa nyumba hizo.
Alisema tangazo la Bw Munene lilimpa afueni mara dufu ikizingatiwa alikuwa amekodisha nyumba ya makazi na nyumbani ya kufanyia biashara katika jengo hilo.
“Wakati huu ambapo biashara ni mbaya kutokana na athari za mkurupuko wa virusi vya corona sikuwa na uhakika kama nitapata Sh16,000 za kulipia nyumba hizo mbili,” akaeleza Bw Muya.
Alisema mapato kutokana na biashara yake yamepungua kutoka Sh1,000 kwa siku hadi Sh200 tangu kisa cha kwanza cha virusi vya corona kutangazwa nchini.
Wengi wa wapangaji wa nyumba za Bw Munene wanafanya kazi katika kampuni za maua, na hivi majuzi walisimamishwa kazi.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, Bw Munene alisema alichukua hatua hiyo kwa kuelewa matatizo wanayopitia wapangaji wake.
Aliongeza kuwa huenda akasongeza muda wa afueni hiyo ya kodi ikiwa hali itaendelea kuwa mbaya zaidi, ikizingatiwa kuwa janga hilo limeathiri uchumi.
“Hali ikiwa mbaya zaidi katika miezi ijayo, nitaongeza muda wa msamaha huo wa kodi ili wapangaji wangu waweza kuelekeza juhudi zao katika harakati za kusaka chakula pekee wala sio kodi,” Bw Munene akaeleza.
Kitendo cha mfanyabiashara huyo kimewachangasha Wakenya katika mitandao ya kijamii ambao wanaomba kuwa landilodi wao waige mfano huo wa kutoa msamaha wa kodi wakati huu mgumu.
“Nadhani landilodi wangu amesikia habari kuhusu kitendo cha Bw Munene na atatupa afueni hii. Nimekuwa mpangaji wake kwa kipindi cha miaka mitano,” akasema Mercy Chirchir kupitia twitter.
“Mungu akabariki Bw Michael Munene, ni vigumu kumpata mtu mwenye kujitolea kama wewe. Hata mabilionea nchini hawawezi kuchukua hatua kama hii,” akaongeza Bw Willie Ben.
Naye Bw Osoro akasema: “Landilodi wangu ni mzuri…. ataiga mfano wa mwenzake.”